Na Abdallah Nassoro-MOI
Timu ya wataalam mbalimbali pamoja na viongozi waandamizi kutoka nchini Gambia siku ya tarehe 29 Novemba, 2024 wameitembelea Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) ili kupata uzoefu wa namna huduma za kibingwa na kibobezi za mifupa, mgongo, ubongo na mishipa ya fahamu na kuona namna ambavyo nchi hizo zinaweza kushirikiana.
Ujumbe huo wa watu 12 ukiongozwa na katibu Mkuu Wizara ya Afya Gambia Prof Omar Jah ulipata fursa ya kupata taarifa za huduma za MOI, mifumo ya Tehama na kutembelea kitengo cha Radiolojia.
“Tunashukuru kwa mapokezi mazuri sana, tumefarijika na tumeona namna ambavyo mmepiga hatua, tumefika kwa ajili ya kujifunza namna ambavyo Mfuko wa Bima ya Afya unafanya kazi hapa nchini na kusaidia kukuza ufanisi katika sekta ya afya” amesema Prof Jah
Menejimenti ya MOI ikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Laurent Lemeri Mchome amesema MOI imefungua milango ya ushirikiano wa kitaifa na Kimataifa ili kukuza utalii tiba nchini na kufikia dhima ya MOI kuwa kituo mahiri cha tiba ya mifupa na ubongo barani Afrika.
“Huduma zetu za kibingwa na kibobezi zimeweza kusaidia wananchi si tu wa Tanzania bali pia wa nchi nyingine za Afrika, tupo tayari kwa ushirikiano ili tuweze kuwajengea uwezo wa taalam wa Gambia katika kutoa huduma za kibingwa na kibobevu za mifupa na ubongo” amesema Dkt. Lemeri