Na Amani Nsello- MOI
Uongozi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) umesema kuwa hakuna mgonjwa wa dharura atayeshindwa kupatiwa matibabu kwa kukosa fedha ikiwa ni utekelezaji wa miongozo na sera ya afya inayoweka kipaumbeke kunusuru maisha ya wangonjwa kwanza.
Hayo yamebainishwa siku ya Ijumaa Novemba 29, 2024 na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt. Laurent Lemeri Mchome wakati akijibu hoja za wagonjwa na ndugu wa wagonjwa wanaopatiwa huduma za matibabu katika taasisi hiyo.
Dkt. Lemeri amesema kuwa taasisi ya MOI imekuwa ikitekeleza na kufuata Sera ya Afya ya kutoa huduma bora za matibabu kwa wagonjwa wote wa dharura.
“Niwahakikishie tu kuwa; Hakuna mgonjwa wa dharura hususani wa ajali za barabarani atakayeletwa hapa hospitalini (MOI) akashindwa kupatiwa huduma za matibabu, kwa sababu hana fedha na mgonjwa kaletwa kwa dharura hapana, atapatiwa huduma za matibabu… Halafu taratibu za kuchangia gharama zitafuata”- amesema Dkt. Lemeri na kuongezea
“Sisi kama hospitali (MOI) tunafuata na kutekeleza Sera ya Afya ya Huduma Kwanza, naomba niwambie pia gharama hizi mnazopatiwa kwenye bill zenu sio halisi, mnachangia tu, gharama zingine zimeshalipwa na serikali…. Kwahiyo nyie mnachangia tu sehemu ndogo ya gharama”
Naye, Elisifa Maimu ndugu wa mgonjwa ameishukuru Taasisi ya MOI hususani Kitengo cha Uangalizi Maalum wa Wagonjwa (ICU) kwa juhudi zao za kumhudumia mgonjwa wake aliyeletwa MOI kwa dharura ya kupata ajali barabarani.