Na Mwandishi wetu- Dar es Salaam.
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) siku ya Disemba 3, 2024 imeshiriki maadhimisho ya siku ya kimataifa ya watu wenye ulemavu duniani yanayofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.
Mgeni rasmi wa maadhimisho hayo alikuwa ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko (Mb) ambaye alimwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb).
Mkuu wa kitengo cha utengamao MOI, Marry Chandeu amesema MOI imeshiriki maadhimisho hayo kwa kutoa ushauri na elimu wa huduma za utengamao (Mazoezi tiba) na Viungo saidizi (Viungo bandia) kwa walemavu mbalimbali waolioshiriki ambao baadhi yao walitibiwa katika Taasisi ya MOI.
Mmoja wa walemavu aliyetibiwa MOI Bi. Neema Seif ameishukuru Taasisi ya MOI kwa kumpatia huduma nzuri mpaka sasa hali yake inaendelea vizuri.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Kukuza Uongozi wa Watu wenye Ulemavu kwa ajili ya Mustakabali Jumuishi na Endelevu”