Na Amani Nsello- MOI
Uongozi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Mubimbili (MOI) umewakumbusha ndugu wa wagonjwa kuwa na tabia ya kufuatilia taarifa sahihi za wagonjwa wao wanaopatiwa huduma za matibabu katika taasisi hiyo.
Wito huo umetolewa leo Jumatano Disemba 04, 2024 na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi wa MOI, Meneja Usafi na Ufuaji, Elizabeth Mbaga wakati akijibu hoja za wagonjwa na ndugu wa wagonjwa katika Taasisi ya MOI wakati wa zoezi l kusikiliza kero, maoni, ushauri na changamoto.
Bi. Mbaga amesema kuwa ni vema ndugu wa wagonjwa kufuatilia taarifa sahihi za wagonjwa wao ili kuepuka mkanganyiko wakati wa kupatiwa huduma za matibabu.
“Ndugu wa mgonjwa unapaswa kufuatilia taarifa sahihi za mgonjwa wako, mfuate muuguzi muulize mgonjwa wangu unampeleka wapi? Wodi namba ngapi? Na asumbuliwa zaidi na nini?… Hiyo itakusaidia kupata zile taarifa sahihi na muhimu za mgonjwa wako”- amesema Bi. Mbaga na kuongezea
“Kama hujamuelewa muuguzi viongozi wapo wafuate waulize, namba za viongozi zipo kila mahali hapa MOI zimebandikwa kwenye mabango”
Naye Salim Ally ndugu wa mgonjwa anayepatiwa matibabu MOI amepongeza uongozi wa MOI kwa kuendeleza kusimamia vizuri suala la usafi.
Taasisi ya MOI kupitia Menejimenti yake imentenga siku za Jumatano na Ijumaa kuanzia saa 5 asubuhi hadi saa 6 mchana kwa ajili ya kupokea maoni changamoto, kero na pongezi kutoka kwa wagonjwa na ndugu wa wagonjwa wanaopatiwa huduma za matibabu katika taasisi hiyo.