Dkt. Mpoki aiomba menejimenti ya MOI iangalie uwezekano wa kutoa huduma saa 24

Na Amani Nsello- MOI

Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) Mhe. Balozi, Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema katika kuendelea kuwapatia huduma bora wagonjwa wa nje na kupunguza msongamano wa wagonjwa ameiomba Menejimenti ya MOI iangalie uwezekano wa kutoa huduma kwa saa 24.

Akizungumza na wajumbe wa menejimenti na wakuu wa vitengo baada ya kukabidhiwa siku ya Disemba, 10, 2024 na aliyekuwa Kaimu Murugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Laurent Lemeri Mchome, Mkurugenzi huyo mpya Dkt. Mpoki ameiomba menejimenti kuangalia kama kuna uwezekano wa kutoa huduma kwa saa 24.

“Wakati unaongea likajia wazo, kwanini tusiangalie uwezekano wa kutoa huduma kwa saa 24, hili likifanyika itasaidia kupunguza muda wa mgonjwa kusubiria huduma” amesema Dkt. Mpoki na kuongeza

“Mtu (mgonjwa) anapotoka Makete na kuja kutibiwa hapa MOI anatakiwa kuproject (kadiria) muda na fedha atakazozitumia kabla, wakati na baada ya kupatiwa huduma za matibabu”

Aidha Dkt. Mpoki amewapongeza watumishi na viongozi wa MOI kwa kazi nzuri na kubwa ambayo wamekua wakiifanya katika kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma nzuri na bora za kibingwa na kibobezi.

Kwa upande wake, Dkt. Lemeri ametoa shukrani kwa Menenjimenti na Watumishi wote wa MOI kwa ushirikiano mkubwa waliompatia kwa kipindi cha miezi 6 alichohudumu kama Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo.

“Kwanza nitoe shukurani kwa Menejimenti na Watumishi wote wa MOI kwa ushirikiano mkubwa mlionipa kwa kipindi cha miezi 6, mmenipa ushirikiano mkubwa sana ambao sikuutegemea”- amesema Dkt. Lemeri na kuongezea

“Taasisi yetu (MOI) ina Wafanyakazi 918 ambao wanaolipwa na Hazina (wenye Ajira za kudumu) lakini pia ina Wafanyakazi 134 wa mkataba (wanaolipwa na Taasisi kwa mapato ya ndani), pamoja na juhudi za serikali lakini bado tuna upungufu wa wafanyakazi 310”

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Lemeri amemweleza Dkt. Mpoki kuwa upo mpango mkakati wa kufanya maboresho ya kitengo cha dharura MOI kwa kushirikiana na Taasisi ya ABBOT Fund ili kuendelea kutoa huduma bora za zenye hadhi ya Kimataifa

About the Author

You may also like these