Na Amani Nsello- MOI
Ndugu wa wagonjwa wametakiwa kulinda na kutunza faragha za wagonjwa wao wanaopatiwa huduma za matibabu kwa kutowapiga picha wakiwa wamelazwa wodini badala yake wawape faraja na matumaini.
Rai hiyo imetolewa leo Jumatano Desemba 11, 2024 na Mwakilishi kutoka Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani na Udhibiti Ubora wa MOI, Afisa Muuguzi Mwandamizi, Bupe Ngunule wakati akijibu hoja za wagonjwa na ndugu wa wagonjwa wanaopatiwa huduma za matibabu katika Taasisi ya MOI.
“Tunajuwa wapendwa wenu (wagonjwa) mnawapenda sana, ila wanapokuwa wodini wamelazwa tafadhalini msiwapige picha, Tulinde na kutunza faragha zao…. Umefika wodini usikimbilie kumpiga picha mgonjwa, mliwaze, mpe matumaini mfariji…. Pengine mdomo wake umekauka mpake mafuta “. Amesema Bi Bupe.
Aidha muunguzi huyo amewasihi ndugu wa wagonjwa kuwasilisha changamoto au kasoro kwa viongozi wa MOI pale wanapokutana na vikwazo katika kupata huduma za matibabu.
Taasisi ya MOI kupitia Menejimenti yake imentenga siku za Jumatano na Ijumaa kuanzia saa 5 asubuhi hadi saa 6 mchana kwa ajili ya kupokea maoni changamoto, kero na pongezi kutoka kwa wagonjwa na ndugu wa wagonjwa wanaopatiwa huduma za matibabu katika taasisi hiyo