Na Erick Dilli- MOI
Madaktari na waaguzi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wamepatiwa mafunzo ya kupunguza vifo kwa njia ya kisasa (5R Rescue Model) ili kudhibiti vifo kwa wagonjwa kabla na baada ya upasuaji.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na Kitengo cha Udhibiti Ubora na Ukaguzi wa Kitabibu MOI kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuboresha Mfumo wa Huduma za Afya (Institute for Health Care Improvement), ili kuwajengea madaktari na wauguzi uwezo wakutumia njia hii katika kupunguza vifo kwa wagonjwa kabla na baada ya upasuaji.
Akifunga mafunzo hayo yaliyofanyika siku 3, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Ubongo MOI, Dkt. Niceforas Mutabasigwa ameeleza umuhimu wa njia hiyo katika kuhakikisha idadi ya vifo inapungua.
“Niwashukuru wote ambao mmejitokeza katika mafunzo haya tuweze kuwajengea huu uwezo pia kwa watumishi wengine, kwani njia hii itasaidia sana kupunguza idadi ya vifo kabla na baada ya upasuaji kwa asilimia 25”-amesema Dkt. Mutabasigwa
Naye muwakilishi kutoka IHI Dkt. Ramadhani Ally ameshukuru madaktari na waaguzi wa MOI kwa ushirikiano wao wakati wa mafunzo.
“Kipekee niwashukuru wote ambao mmejitokeza wakati wa mafunzo haya kwani kwa ujuzi huu ambao mmeupata utasaidia kufukia malengo ambayo tumeweka ili kuhakikisha tunapunguza idadi ya vifo kabla na baada ya upasuaji”-amesema Dkt. Ramadhani