MOI kuondoa foleni ya wagonjwa kumuona daktari

Na Stanley Mwalongo- MOI

Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Majeruhi na Ubongo Muhimbili (MOI) imesema ipo mbioni kuanzisha mfumo wa kidijitali wa kuweka ahadi ya kuonana na daktari bingwa husika kwa lengo la kuwapunguzia foleni wagonjwa wanaopata huduma MOI.

Hayo yamebainishwa leo Disemba, 13, 2024 na Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Ubongo Dkt. Laurent Lemeri (kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu) katika zoezi la kupokea maoni, kero, ushauri, changamoto na pongezi kutoka kwa wagonjwa na ndugu wa wagonjwa wanaopata huduma MOI.

Dkt. Lemeri amesema mfumo huo utawaondolea adha na usumbufu wagonjwa ya kupanga foleni muda mrefu na utasaidia kutoa huduma kwa haraka zaidi.

“Siku si nyingi tutapunguza foleni za wagoniwa wanaopata huduma MOI, tutatumia mfumo wa kidijitali ambapo kupitia simu zenu mtafanya ‘booking’ za kuwaona madaktari, mtapata control namba kwa ajili ya kulipia, na utalipia huko huko nyumbani huku ukija unaenda moja kwa moja kwenye chumba cha daktari kwa ajili kumuona” . Na hii haitakuwa peke yake, hata huduma nyingine kama vile vipimo vya maabara pamoja na radiologia nk utaweza kulipia na kufika moja kwa moja kupata huduma hizo amesema Dkt. Lemeri

Aidha Dkt. Lemeri amewashauri wananchi kujiunga na kuwa mabalozi wa bima ya afya kwa wote pindi itakapoanza kutumika kwani kama watanzania wote wakijiunga mfuko utakuwa na nguvu kubwa ya kutoa huduma nyingi.

Kwa upande wake ndugu wa mgonjwa anayepata huduma MOI Bw. Mbalasi Musa amewashukuru madaktari, wauguzi na watoa huduma wote wa MOI kwa kutoa huduma bora na nzuri kwa wagonjwa wanaotibiwa MOI.

About the Author

You may also like these