Mkurugenzi mtendaji MOI aomba wadau zaidi wajitokeze kusaidia matibabu ya watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi

Na Amani Nsello- MOI

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya amewaomba wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia matibabu ya watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi wanaoendelea na matibabu katika Taasisi ya MOI.

Wito huo aliutoa siku ya Desemba, 16, 2024 wakati wa hafla ya kukabidhi tuzo ya kutambua mchango wa Wakenya wawili Zarnat Datoo na Jamie Satchell waishio Uingereza waliochangia matibabu ya watoto 10 wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.

Dkt. Mpoki alisema watoto hao wanahitaji msaada zaidi wa matibabu kwa sababu wengi wao hutoka katika familia duni kutokana mzigo wa kuwalea kuachwa mikononi kwa akina mama baada ya kukimbiwa na waume zao.

“MOI ni nyumbani kwenu, karibuni muda wowote, tunawashukuru sana kwa mchango wenu kwa kufanikisha matibabu ya watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi… Tunawaomba mchango huu usiwe wa mwisho, muendelee kuwa na moyo huo wa kutoa na kusaidia” alisema Dkt. Mpoki na kuongeza

“Nitoe wito kwa Watanzania, mashirika, makampuni na taasisi za serikali kujitokeza kuendelea kusaidia matibabu ya watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi wanaohudhuria kliniki katika taasisi ya MOI”

Kwa upande wake, Bi. Zarnat alisema kuwa yeye na mume wake Jamie Satchell wamekuwa wakitoa msaada wa matibabu kwa watoto waishio katika mazingira magumu nchi mbalimbali duniani.

“Mimi na mume wangu sio kwamba ni matajiri sana! Hapana, tunasaidia kidogo tulichobarikiwa na Mungu, ni utamaduni wetu wa kusaidia hususani kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu… Kwa hapa MOI hii ni awamu ya nane tunatoa msaada kwa watoto hao, tutaendelea kutoa msaada kwa kadri tutakavyoweza ili kuokoa maisha ya watoto” alisema Bi. Zarnat

About the Author

You may also like these