Na Abdallah Nassoro – MOI
Menejimenti ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) leo Desemba, 20, 2024 imekagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi ndani ya taasisi hiyo, huku ikiagiza wakandarasi kuongeza kasi ya ujenzi kwa kufanya kazi kwa saa 24.
Menejimenti hiyo ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendajiwa MOI Dkt. Mpoki Ulisubisya ilitembelea mradi wa ukarabati wa jengo la iliyokuwa hospitali ya Tumaini, ambapo huduma mbalimbali za MOI zitahamia katika eneo hilo ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa kupunguza msongamano wa wagonjwa katika eneo la sasa la kutolea huduma kwa wagonjwa wa nje (OPD).
“Fanyeni kazi saa 24 ili mradi huu ukamilike kwa wakati, viongozi wenzangu naona huu mradi ulikuwa ukamilike jana, ukiangalia ule msongamano wa wagonjwa unatamani huu mradi ukamilike sasa hivi, nadhani inawezekana kufanya kazi saa 24” amesema Dkt. Mpoki
Menejimenti hiyo pia ilikagua mradi wa kituo cha kuzalisha Oksijeni kwa kutumia gesi uliokamilika kwa asilimia 100 pamoja na mradi wa ujenzi wa eneo la kutolea huduma kwa wagonjwa wa nje (OPD) uliofikia asilimia 7 za ujenzi.
“Mjipange kufanya kazi saa 24 ili mradi uweze kukamilika kwa wakati, jukumu letu ni kusimamia miradi hii ikamilike kwa wakati ili tuwee kutatua changamoto ya msongamano wa wagonjwa”
Kwa upande wake Kaimu Meneja Ufundi na Matengenezo wa MOI Manyori Kapessa amesema mradi wa mtambo wa gesi kwa ajili ya kuzalisha Oksijeni umegharimu Tsh. 1.6 bilioni wakati ujenzi wa OPD mpya utagharimu Tsh. 11 bilioni.