Na Amani Nsello-MOI
Uongozi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) umewakumbusha ndugu wa wagonjwa kufuatilia ankara za malipo za wagonjwa wao ili kuepuka kulimbikiza madeni ya gharama za matibabu.
Hayo yamebainishwa jana Ijumaa, Desemba 20, 2024 na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi wa MOI, Afisa Muuguzi Mwandamizi wa MOI, Furaha Godfrey wakati akijibu hoja na maoni ya wagonjwa na ndugu wa wagonjwa wanaopatiwa huduma za matibabu katika taasisi hiyo.
Bi. Furaha amesema kuwa ni vema ndugu wa wagonjwa kila wanapoenda kuwajulia hali wagonjwa wao wafike ofisi za uhasibu kuulizia ankara zao ili kupunguza madeni ya huduma za matibabu.
“Kila mnapokuja kuwajulia hali wagonjwa wenu tafadhalini mfike ofisi za uhasibu kujua bill (ankara) zenu… Mkifanya hivyo mara kwa mara itawasaidia kujua gharama za matibabu za huduma walizopatiwa wagonjwa wenu, lakini itawasaidia kupunguza mrundikano wa madeni ya gharama za matibabu” amesema Bi. Furaha
Kwa upande wake, ndugu wa mgonjwa kutoka Dodoma, Keneth Machao amewashukuru Madaktari na wauguzi wa kitengo cha dharura kwa kumpokea vizuri mgonjwa wake na kumpatia huduma za matibabu kwa haraka.
“Tulipewa Rufaa kutoka Benjamin Mkapa Dodoma, tulifika hapa saa 8 usiku, licha ya kufika usiku huo wa manane tulikuta Madkatari hapo Emergency (Kitengo cha Dharura), mgonjwa wangu walimpokea vizuri , alizungukwa na Madaktari 8 na manesi, walimhudumia kwa haraka sana, asanteni sana MOI” amesema Bw. Keneth
Taasisi ya MOI kupitia Menejimenti yake imetenga siku za Jumatano na Ijumaa kuanzia saa 5 asubuhi hadi saa 6 mchana kwa ajili ya kusikiliza kero, maoni, changamoto na pongezi kutoka kwa wagonjwa na ndugu wa wagonjwa wanaopatiwa huduma za matibabu katika taasisi hiyo.