mtoto wa wiki moja afanyiwa upasuaji wa kichwa kikubwa

Mtoto wa wiki moja afanyiwa upasuaji wa kichwa kikubwa MOI

Na Mwandishi wetu

Taasisi ya Mifupa Muhimbili MOI imeendelea kuandika historia katika utoaji huduma za kibingwa hapa nchini ambapo imefanikiwa kumfanyia upasuaji wa kichwa kikubwa mtoto mwenye umri wa wiki moja.

Upasuaji huo umefanywa katika kambi maalum ambapo zaidi ya watoto 24 wamefanyiwa upasuaji wa kuzibua njia za maji kichwani pamoja na kuwekewa mirija ya kutoa maji kichwani na kuyapeleka Tumboni.

Daktari bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya fahamu MOI Dkt. Hamisi Shabani amesema wamefanikiwa kufanya upasuaji kwa mtoto mwenye umri mdogo kutokana na uwepo wa wataalam wabobezi na uwepo wa vifaa vya kisasa vya teknolojia ya juu katika Taasisi ya MOI.

“Tunaishukuru Serikali yetu ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mh Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanya uwekezaji mkubwa kwenye vifaa tiba katika taasisi yetu, uwepo wa vifaa vya kisasa umepelekea ubora wa huduna zetu kuimarika.” Alisema Dkt. Shabani

Pia, Dkt Shabani ameushukuru uongozi wa Taasisi ya MOI chini ya Dkt Respicious Boniface pamoja na wadau wengine kwa kuhakikisha huduma bora zinaendelea kupatikana kwa watanzania na raia wa mataifa mengine.

Taasisi ya MOI imeendelea kuwa mfano na kinara katika kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za kibingwa bila kulazimika kufuata huduma nje ya nchi.

About the Author

You may also like these