MOI yahimiza wananchi kuwa mabalozi wa bima za afya.

Abdulaziz Seif- MOI

Menejimenti ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo (MOI) imewataka wananchi kuwa mabalozi wazuri wa kuhamasisha wenzao kujiunga na mfuko wa bima ya afya ili kupunguza gharama za matibabu pindi wanapougua.

Akijibu malalamiko kutoka kwa wateja waliolalamikia gharama gharama za Matibabu, Kaimu Mkurugenzi wa MOI Dkt. Lemeri Mchome, amewataka wananchi kujiunga na bima ya afya kabla hawajapata matatizo ya afya na pia wawe mabalozi wazuri wa kuhamasisha wananchi wengine kujiunga.

“Nawaomba wananchi kujiunga na bima ya afya mapema ili kupunguza gharama za matibabu, wagonjwa wengi wanaletwa MOI hawana bima za afya hivyo inawalazimu watumie fedha taslimu jambo ambalo linawapa changamoto kumudu gharama za matibabu..

Tuwe mabalozi wazuri kwa wengine kuhusu swala la bima za afya na pia tuwahimize ndugu zetu boda boda kulipia bima maana wao ndio wahanga wakubwa wa ajali za barabarani” amesema Mchome

Taasisi ya MOI imejiwekea utaratibu wa kusikiliza kero, maoni, ushauri na pongezi kutoka kwa wananchi ili kuboresha huduma kila siku ya Jumatano kuanzia saa 5:30 hadi saa 6:00 na Ijuma muda huo huo.

About the Author

You may also like these