matibabu ya kibingwa

MOI yaandika historia ya matibabu ya kibingwa nchini

Na Mwandishi wetu- MOI

Taasisi ya tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) imeandika historia katika matibabu ya kibingwa hapa nchini ambapo huduma mpya ya kibingwa ya matibabu ya maumivu sugu ya mgongo na kichwa bila upasuaji imezinduliwa na kuwanufaisha zaidi ya wagonjwa ishirini (20).

Huduma hiyo ambayo haipo hapa nchini imeanzishwa kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya MOI na hospitali ya YASHODA- India.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respicious Boniface amesema MOI imeanzisha huduma hii ili kuendelea kutekeleza agizo la Serikali ya awamu ya Sita la kuhakikisha Tanzania inakuwa kituo cha utalii wa matibabu (Medical Tourism).

“Kama mnavyofahamu Mh Rais, Dkt Samia Suluhu Hassan ana msukumo mkubwa wa kuifanya nchi yetu kuwa kitovu cha utalii wa matibabu katika ukanda wa Afrika Mashariki kati na kusini, hivyo kuanza kwa huduma hii ni sehemu ya mkakati wetu wa kutekeleza kwa vitendo maono hayo ya Mh Rais” Alisema Dkt Boniface

Naye mjumbe wa kamati ya Kitaifa ya utalii wa matibabu Bw. Abdulmalik Mollel amesema huu ni muda muafaka kwa Tanzania kuwa kituo cha utalii wa matibabu kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya awamu ya Sita kwenye sekta ya afya ambapo huduma nyingi za kibingwa na kibobezi zinapatikana hapa nchini.

Kwa upande wake daktari bingwa wa upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu kutoka hospitali ya YASHODA-India Dkt. Ravi Suman Reddy amesema ushirikiano kati ya MOI na hospitali ya YASHODA utaleta manufaa makubwa kwa watanzania na mataifa mengine ya Afrika Mashariki na kati ambako huduma hii haipatikani.

Daktari bingwa wa upasuaji wa mgongo na ubongo MOI, Dkt. Nicephorus Rutabasibwa amesema kambi hii itakuwa na matokeo chanya kwa huduma za kibingwa hapa nchini kwani huduma hizi zitaendelea kutolewa MOI hata baada ya wataalamu kutoka nchini India kuondoka na hivyo kuwaondolea usumbufu wagonjwa kufuata huduma nje ya nchi.

About the Author

You may also like these