Madaktari bingwa kutoka China

Madaktari bingwa kutoka China

Taasisi ya tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) imepokea timu ya madaktari bingwa kutoka Serikali ya Jamhuri ya watu wa China ambao watatoa huduma za kibingwa katika Taasisi za MOI, MNH, JKCI na hospitali ya rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH) kwakipindi cha miaka 2.

Mnamo mwezi septemba mwaka 2021, Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya iliingia mkataba namba 26 wa ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya watu wa China, mkataba huo pamoja na mambo mengine ulijikita katika mafunzo ya muda mrefu na mfupi pamoja na kuleta madaktari bingwa kutoka China kutoa huduma katika hospitali za kibingwa hapa nchini.

Akizungumza katika hafla ya kupokea madaktari bingwa hao katika Taasisi ya MOI, Mkurugenzi Mtaendaji wa MOI Dkt. Respicious Boniface amesema ujio wa madaktari bingwa hao ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha huduma za kibingwa ambapo pamoja na kutoa huduma kwa wagonjwa madaktari hao watafundisha wanafunzi.

“Ujio wa wataalamu hawa una tija kubwa kwa Taasisi yetu na kwa nchi kwa ujumla kwani watafanya upasuaji kwa kushirikiana na madaktari bingwa wazalendo jambo ambalo litapelekea kubadilishana uzoefu na kupeana mbinu za kisasa, pia watatoa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi kwani moja ya malengo ya MOI ni kutoa mafunzo” Alisema Dkt. Boniface

Kwa upande wake Kiongozi wa timu ya madaktari bingwa kutoka China Dkt. Meng Yong amasema ni heshima kubwa kupata fursa ya kufanya kazi Tanzania na kuwa hudumia watanzania kwa kipindi cha miaka miwili ambapo pia watapata nafasi ya kubadilishana uzoefu na madaktari bingwa wenzao wa Tanzania na kujifunza mambo mengi.

Muwakilishi wa Wizara ya Afya Tanzania Dkt. Vumilia Liggyle amesema ushirikiano baina ya Serikali hizi mbili (Tanzania na China) ni wa kihistoria kwani una zaidi ya miaka 50 na umekuwa ukienziwa kizazi hadi kizazi jambo ambalo limekuwa likiwanufaisha wataalamu kwenda nchini China kupata mafunzo na madaktari bingwa kutoka China kuja hapa nchini kutoa huduma.

Ujio wa madaktari bingwa hawa ni sehemu ya mkakati wa Serikali ya Awamu ya 6 inayo ongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha huduma zote za kibingwa zinapatikana hapa nchini na kuifanya Tanzania kuwa kituo cha matibabu barani Afrika.

About the Author

You may also like these