Na Mwandishi wetu
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imepeleka madaktari bingwa na wabobezi wanne nchini Uingereza kupata mafunzo ya kibobezi ya juu (Super specialization) ya upasuaji wa magoti na mabega kwa njia ya matundu (Knee and Shoulder Athroscopy).
Mafunzo hayo yameratibiwa na MOI kwa ushirikiano na Taasisi ya Smith and Nephew ,Chama cha Madaktari bingwa wa mifupa nchini Uingereza na Taasisi ya St. Roch Group ya Uingereza.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Laurent Lemeri Mchome amesema mafunzo haya ni mkakati wa Taasisi ya MOI wa kuhakikisha inaendelea kuwa kinara katika utoaji wa huduma bora za upasuaji wa kibobezi wa magoti na mabega kwa njia ya matundu hususani kwa wanamichezo.
“Mashindani ya Afcon yatafanyika 2027 hapa nchini hivyo mafunzo haya yanawajengea uwezo zaidi madaktari bingwa na wabobezi wetu ya kuendelea kutoa huduma bora kwa wanamichezo kutoka nchini mbalimbali baranı Afrika watakaoshiriki katika mashindano hayo” amesema Dkt. Mchome
Taasisi ya MOI inaendelea kutekeleza kwa vitendo maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha huduma za matibabu ya kibingwa na kibobezi ya mifupa, ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu yanawafikia wananchi na kuvuka mipaka kufikia nchi mbalimbali.