Na Amani Nsello- MOI
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dkt. Said Ally Mohamed amemjulia hali Clement Jackson manusura wa ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa Kariakoo ambaye ni mtahiniwa wa Kidato cha Nne 2024 anayepatiwa matibabu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI).
Dkt. Mohamed akiambatana na Balozi Dkt. Salim Othman Hamad, Msaidizi wa Rais anayeshughulikia masuala ya Siasa, amemjulia hali mwanafunzi huyo wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Charambe ya Temeke Jijini Dar es Salaam, Siku ya Novemba 19, 2024 katika Taasisi ya MOI.
Dkt. Mohamed amesema wao kama NECTA watatumia kanuni za Baraza hilo katika kushughulikia suala lake, na kwamba mwanafunzi huyo hatapoteza haki yake ya mtihani.
“Kuhusu mtahiniwa huyu, Baraza lina taratibu zake litaandaa taarifa zake na kuchukua hatua stahiki. Lakini niseme tu, tumefarijika kuona katika mitihani yake ya wiki ya kwanza ameweza kufanya yote na alikuwa anatarijia kufanya mtihani tarehe 21 mtihani wa Practical Biology 2B” Amesema Dkt. Mohamed na kuongezea
“Ni mwanafunzi ambaye alikuwa na juhudi na ajali (ajali ya kuporomoka jengo la ghorofa la Kariakoo) imemkuta, lakini Baraza (NECTA) litampa haki yake kadri inavyostahiki”.
Kwa upande wake mwanafunzi Clement Jackson manusura wa ajali hiyo, amemshukuru Katibu Mtendaji wa NECTA kwa kumjulia hali na kumpa pole, na kumuomba kushughulikia suala lake kwa mujibu wa kanuni za Baraza zinavyoelekeza.