Na Erick Dilli- DODOMA
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeshiriki katika wiki ya kuzuia magonjwa yasioambukiza kwa kuendelea kutoa elimu pamoja na ushauri wa namna ya kujiepusha na magonjwa hayo kwa wakazi wa Jiji la Dodoma.
Wiki ya Maadhimisho hayo imefikia kilele leo Jumamosi Novemba 16, Jijini Dodoma ambapo yalitanguliwa na mazoezi ya kutembea kuanzia Makao Makuu ya Polisi Dodoma na kuishia Viwanja vya Wajenzi.
Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule amewashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa kipindi chote cha wiki ya magonjwa yasioambukiza na kuwahimiza wananchi hao kuhusu umuhimu wa kufanya mazoezi.
“Nishukuru hospitali zote ambazo zimeungana na wizara ya afya katika kutoa huduma ya elimu, pamoja na vipimo kwa wakazi wa Dodoma, kwani huduma hizi zilikuwa zinatolewa bure na pia nishukuru wananchi wa Dodoma kwa kujitokeza na kupata huduma hizo” amesema Mhe. Senyamule na kuongezea
“Mtu asiyefanya mazoezi wakati ana uwezo wa kufanya mazoezi ni mtu asiyejithamini, kujijali na asiyejipenda, kwa sababu mwisho wa siku mtu atapata magonjwa ambayo angeweza kuyazuia kwa kufanya mazoezi”
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Tiba Wizara ya Afya, Dkt. Hamad Nyembea, ametaja baadhi ya magonjwa hayo kuwa ni kisukari, shinikizo la damu, selimundu, magonjwa ya afya ya akili na magonjwa ya moyo, ambapo amesema yanaweza kuzuilika kwa kushughulisha mwili na kuzingatia ulaji sahihi.