Dkt. Mpoki awashauri watanzania kujiunga vitita vya bima ya afya ili kumudu gharama za matibabu.

Na Amani Nsello- MOI

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya amewashauri Watanzania kujiunga na mifuko ya bima ya afya ili iwasaidie kupunguza ukali wa gharama za matibabu pindi wanapougua.

Dkt. Mpoki ametoa ushauri huo leo Ijumaa Januari 24, 2025 wakati akijibu hoja na changamoto za wagonjwa na ndugu wa wagonjwa eneo la kusubiria huduma (MOI Clients Lounge).

Amesema kuwa ili kupunguza ukali wa gahrama za huduma za matibabu ni muhimu kwa kila mtanzania kujiunga na mifuko ya bima ya afya.

“Sisi kama jamii tukumbushane tu tunatakiwa kujiunga na hii mifuko ya bima ya afya ili bima ipunguze makali wa gharama wa huduma za matibabu pindi tutakapougua”amesema Dkt.Mpoki na kuongeza kuwa

“Ni lazima kwa mgonjwa kuchangia gharama za matibabu kwasababu kuna vifaa tiba kama vipandikizi tunaagiza nje ya nchi, hivyo ili huduma ili iwe endelevu ni lazima kwa wagonjwa kuchangia gharama za matibabu, na hapa ndipo umuhimu wa bima ya afya unapojitokeza”

Aidha, Dkt. Mpoki amesema kuwa Taasisi ya MOI kufikia Februari Mosi, mwaka huu (2025), mgonjwa ambaye atatakiwa kufanyiwa upasuaji atapewa mchanganuo wote wa gharama za upasuaji huo ili kupunguza usumbufu wa kila mara kupewa ankara mpya.

Kwa upande wake, ndugu wa mgonjwa kutoka Songea, Edward Mhagama amewashukuru na kuwapongeza madaktari na wauguzi wa MOI kwa uvumilivu wao na kujitoa kwao kuwahudumia wagonjwa katika taasisi hiyo.

About the Author

You may also like these