MOI: Waleteeni wagonjwa wenu vyakula vyenye kuongeza damu

Na Amani Nsello- MOI

Ndugu wa wagonjwa wenye wagonjwa wanaopatiwa huduma za matibabu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wameshauriwa wanapowatembelea wagonjwa wao kuwapelekea vyakula vyenye kuongeza damu kutokana na mahitaji makubwa ya damu ili kukabiliana na upungufu wa damu mwilini.

Ushauri huo umetolewa leo Jumatano Januari, 22, 2025 na Afisa Muuguzi wa MOI kutoka Kitengo cha Wagonjwa wenye Mahitaji Maalum (HDU), Idrisa Thabiti wakati akijibu maoni na hoja mbalimbali eneo la kusubiria huduma (MOI Clients’ Lounge).

Bw. Thabiti ameshauri kuwa ndugu wa wagonjwa wanapokwenda kuwajulia hali wagonjwa wao waende na vyakula vya kuongeza damu kwa sababu wengi wao hufanyiwa upasuaji mkubwa ambao hupelekea upotevu wa damu nyingi.

“Tunashauri ndugu wa wagonjwa wanapokuja hapa hospitalini (MOI) kuwaona wagonjwa wao wawaletee vyakula vya kuongeza damu, kwa sababu wagonjwa walio wengi hapa hufanyiwa upasuaji hivyo husababisha kupoteza kwa damu nyingi… vyakula vya mbogamboga za majani (matembele, mchicha, kabichi), pia nyama, maini na vyakula vyote vyenye madini ya ‘iron’ (madini ya chuma)”- amesema Bw. Thabiti

Vilevile Bw. Thabiti ameshauri Watanzania kuendeleza utamaduni wa kufika katika vituo vya afya, zahanati na hospitali kwa ajili ya kuchangia damu kwani uhitaji ni mkubwa wa damu hizo.

Kwa upande wake, ndugu wa mgonjwa Isaya Saulo anayepatiwa huduma za matibabu MOI, ameshukuru uongozi wa MOI kwa kusikiliza maoni, changamoto na kero kutoka wagonjwa na ndugu wa wagonjwa na kuzitolea majibu kwa uwazi.

Taasisi ya MOI kupitia Menejimenti yake, imetenga siku ya jumatano na ijumaa kuanzia saa 5 asubuhi hadi saa 6 mchana kwa ajili ya kusikiliza maoni, kero, changamoto, ushauri na pongezi kutoka kwa wagonjwa na ndugu wa wagonjwa wanaopatiwa huduma za matibabu katika taasisi hiyo.

About the Author

You may also like these