Na Amani Nsello-MOI
Katika kuendeleza malezi bora kwa mtoto, watumishi wa Taasisi ya Tiba ya mifupa Muhimbili (MOI) wameshauriwa kutenga nafasi kwa watoto wao kucheza michezo ili kuwakuza kiakili, kimwili na kiafya.
Ushauri huo umetolewa leo Jumatano Agosti 28, 2024 na Afisa Ustawi wa Jamii Stella Kihombo wa MOI wakati akizungumza na baadhi ya wauguzi wa taasisi hiyo ikiwa ni muendelezo wa mafunzo ya malezi bora kwa watoto katika ukumbi wa mikutano jengo jipya la MOI.
Stella amesema kwamba watumishi wanapaswa kuwapa nafasi watoto wao kucheza michezo yao ya kitoto ili kuwajengea uwezo wa kukua vyema kiafya, kiakil na kimwili.
“Sisi majumbani kwetu sidhani kama tunawapa nafasi watoto wetu kucheza michezo yao ya kitoto, sebuleni kwetu tuna makochi ya letha, unamkataza mtoto kucheza kwenye makochi kuwa atayaharibu, utasikia mzazi anamwambia mtoto usichezee makochi, tunathamini sana samani kuliko michezo ya watoto wetu” Amesema Stella
“Nyumba zetu hata nafasi za kuchezea watoto hakuna, kote tumepanda maua na watoto unawapiga marufuku kuchezea kwenye bustani za maua, tusifanye hivyo tuwaache watoto wacheze ili waweze kukua vyema kiakili, kimwili na kiafya” Amesisitiza Stella
Aidha, Stella ameelezea vitu vingine muhimu katika malezi, makuzi na maendeleo ya mtoto kuwa ni afya, elimu, kujali, utambulisho, familia na jamii.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi MOI, Fidelis Minja amesema kuwa Maafisa Ustawi wa Jamii pia wanao wajibu wa kuwafundisha watumishi wa MOI masuala ya ndoa kwani kwa sasa familia nyingi zinapitia changamoto za ndoa, hivyo ni jambo jema kwa watumishi wapewe ushauri nasaha kuhusiana na ndoa.