Na Amani Nsello- MOI
Wataalam wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wameshauriwa kushirikisha jamii katika tafiti za matibabu ya majeruhi wa kichwa na kuvunjika migongo kwa ajili ya kupata taarifa jumuishi zitakazopelekea matokeo chanya katika mnyororo wa matibabu ya wagonjwa hao.
Ushauri huo umetolwa leo Julai 1, 2025 na Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa Ubongo MOI, Dkt. Lemeri Mchome kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MOI wakati akifungua mafunzo ya Utafiti wa Kitaaluma wa kina kwa Upasuaji wa Ubongo Kimataifa na ushirikishwaji wa jamii katika Utafiti wa Majeraha ya Ubongo na Mishipa ya Fahamu.
Dkt. Lemeri amesema, mafunzo haya yamekuja wakati muafaka ambapo kuna uhitaji mkubwa wa kuunganisha mnyororo wa matibabu kuanzia hospitalini mpaka waathirika wanaporudi katika jamii.
“Tafiti nyingi katika nyanja hii zimekuwa zikijikita katika mazingira ya hospitali bila kufuatilia upande wa pili mara wanaporudi katika familia hivyo kupelekea kukosa taarifa muhimu zitakazoweza kutumika kutengenezea sera za taasisi zenye tija zaidi kwa wagonjwa….Ni vema wataalam kuchukua ujuzi huu muhimu na kuanza kuufanyia kazi ili matokeo ya tafiti hizi za kipekee yakaboreshe afya na maisha ya wanajamii wetu, zipo taarifa nyingi kwenye jamii ambazo zinahitajika kutumiwa ili kuleta mageuzi katika huduma kwa wagonjwa hawa maheruhi” amesema Dkt. Lemeri na kuongeza kuwa
“Baada ya mafunzo haya mtaenda kwenye jamii kwa ajili ya kufanya tafiti, sasa tafiti zenu lazima muwashirishirikishe wadau (jamii), hao ndiyo wataowapa uhalisia kwani wao wamebeba hisia na changamoto zote wanazifahamu…nyakati za sasa tafiti ni nyenzo muhimu kupata suluhisho la kudumu kwaa jamii hususani tafiti za huduma za upasuaji wa ubongo wa majeraha na mishipa ya fahamu”
Kwa upande wake, Profesa Mbobezi wa Huduma za Uuguzi na masuala ya Utafiti wa majeraha ya ubongo na mishipa ya fahamu,
Prof. Charlie Whiffin kutoka Chuo Kikuu cha Derby cha nchini Uingereza, amesema kwamba amefurahishwa na mapokezi ya wenyeji wake na anajisikia kama yupo nyumbani kwao na atatumia maarifa yake katika kuwajengea uwezi Wataalam hao ili waweze kufanya tafiti zao kwa ufasaha zaidi.
Mafunzo hayo ya siku 4 yameanza leo Julai 1, 2025 na yatafikia tamati Julai 4, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano uliopo MOI.