Na Amani Nsello- MOI
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imetamatisha maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa kutoa vyeti vya pongezi kwa watumishi hodari waliokuwa mfano wa kuigwa katika utoaji wa huduma bora kwa wateja.
Akizungumza wakati wa kufunga maadhimisho hayo leo Ijumaa Oktoba 10, 2025 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt. Anthony Assey, amesema wiki ya huduma kwa wateja ni muhimu katika kuimarisha ari ya utoaji huduma bora na kujenga mahusiano mazuri kati ya taasisi na wananchi.
“Tunapoadhimisha wiki kama hii, tunapata nafasi ya kujitathmini na kuona wapi tunafanya vizuri na wapi tunapaswa kuboresha. Watumishi waliotukuzwa leo ni mfano wa kuigwa katika kuonesha ubunifu, nidhamu, na moyo wa kujitoa kwa ajili ya wagonjwa,” amesema Dkt. Anthony
Kwa upande wake, Kaimu Meneja Udhibiti Ubora na Huduma kwa Wateja wa MOI, Dkt. Kennedy Nchimbi, amesema taasisi hiyo itaendelea kuwekeza katika mafunzo na motisha ili kuhakikisha wateja wanapata huduma bora zaidi kila siku.
“Tunataka kila mteja anayeingia MOI ajisikie kuthaminiwa. Hii wiki imetupa fursa ya kujifunza, kusikiliza mrejesho kutoka kwa wateja, na kutambua wale wanaotoa huduma kwa viwango vya juu. Tunawapongeza sana watumishi wetu hodari,” alisema Dkt. Nchimbi.
Maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa mwaka huu yamebeba kaulimbiu isemayo Dhamira Inayowezekana ‘Mission Possible’ na yamehusisha shughuli mbalimbali ikiwemo elimu kwa wateja, kukusanya maoni, malalmiko, maoni na pongezi kutoka kwa wagonjwa na ndugu wa wagonjwa.