wagonjwa wanaotibiwa MOI watakiwa kujihadhari na vishoka

Na Amani Nsello- MOI

Wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wametakiwa kujihadhari na vishoka wakati wa kupatiwa huduma za matibabu katika taasisi hiyo kwa kuhakikisha malipo yote yanafanywa kupitia namba ya udhibiti (control number).

Hayo yamebainishwa siku ya Oktoba 30, 2024 na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa MOI, Orest Mushi wakati akijibu hoja za wagonjwa na ndugu wa wagonjwa wakati wa kusikiliza maoni, kero na changamoto.

Mkurugenzi Mushi amesema kuwa taasisi ya MOI haina utaratibu wa kulipia huduma za matibabu kwa fedha taslimu bali huduma zote za matibabu zinalipiwa kwa mfumo maalum kwa kutumia namba ya udhibiti (Control number).

“Hapa MOI hatuna utaratibu wa kupokea fedha ‘cash’, huduma zote za matibabu zinalipiwa kwa kutumia ‘control number’ zinazotolewa na Wahasibu, jiepusheni na vishoka, ni muhimu mkafuata utaratibu uliopo wa kulipia huduma za matibabu”. amebainisha na kuongezea kuwa

“Tumekuwa tunapokea malalamiko kwa baadhi ya watumishi wetu wa MOI kupokea fedha nje ya utaratibu uliopo, msikubali kutoa fedha tasilimu ili mpatiwe huduma za matibabu”

Naye, Flora Mwayoyo ndugu wa mgonjwa anayepatiwa huduma za matibabu MOI, amewashukuru wauguzi wa taasisi hiyo kwa kumpokea na kumpatia huduma nzuri za matibabu ndugu yake.

“Nilikuja juzi hapa MOI, nashukuru walinipokea vizuri pale kitengo cha dharura (EMD), walimhudumia vizuri na siku iliyofuata walimhamishia wodini, kule kuna nesi anaitwa Grace nilisoma kitambulisho chake, namshukuru sana alimhudumia vizuri na kwa upendo mgonjwa wangu”. Amesema Flora

Taasisi ya MOI imetenga siku za Jumatano na Ijumaa kuanzia saa 5 asubuhi hadi saa 6 mchana kwa ajili ya kusikiliza kero, changamoto, maoni na pongezi kutoka kwa wagonjwa na ndugu wa wagonjwa wanaopatiwa huduma za matibabu katika taasisi hiyo

About the Author

You may also like these