Wagonjwa 12 wafanyiwa upasuaji wa uti wa mgongo kwa njia ya matundu MOI

Na Abdallah Nassoro-MOI

Wagonjwa 12 wamefanikiwa kufanyiwa upasuaji wa uti wa mgongo kwa njia ya matundu (endoscope) Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wakati wa kambi maalum ya matibabu ya kibingwa iliyomalizika jana Februari, 08, 2025.

Kwa upasuaji huo MOI imekuwa taasisi ya kwanza nchini kutoa huduma hizo baada ya kupokea mashine ya kisasa (Endoscope tower) ya kufanyia upasuaji huo yenye thamani ya Tsh. 500 Milioni kutoka kampuni ya Joimax ya nchini Ujerumani.

Mratibu wa kambi hiyo daktari bingwa mbobezi wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu Dkt. Hamisi Shabani amesema upasuaji huo umefanyika kwa mafanikio makubwa na hali za wagonjwa zinaendelea vizuri.

“Wagonjwa wote 12 wamefanyiwa upasuaji na wanaendelea vizuri, hii inaifanya Taasisi ya MOI kuwa kinara katika utoaji wa huduma za upasuaji wa uti wa mgongo kwa matundu katika ukanda wa Afrika mashariki, kati na kusini na kuchagiza dhana ya tiba utalii” amesema Dkt. Shabani na kuongeza kuwa

“kwa niaba ya timu ya wataalam tunawashukuru wakufunzi wetu hawa kwa kutujengea uwezo ili nasi tufanye upasuaji huu wa kisasa unatumia muda mchache wa kufanya upasuaji, pia mgonjwa anakaa muda mfupi wodini na hii ndiyo teknolojia ya inayotawala dunia kwa sasa”

Kwa upande wake Mkufunzi wa mafunzo kutoka Chuo Kikuu cha Tiba cha Weill Cornel cha nchini Marekani Dkt. Don Park ameipongeza Taaisis ya MOI kwa kuwa tayari kuwekeza katika ujuzi wa wataalam wake na kuahidi kuendelea kuwajengea uwezo katika huduma za kibingwa na kibobezi ili waendane na mabadiliko ya teknolojia duaniani.

“Upasuaji wa wagonjwa wote umeenda vizuri na sisi kama wakufunzi tumejiridhisha kuwa madaktari wa MOI wanaweza kuendelea kutoa huduma hiyo kwa wagonjwa bila matatizo yyoyote…imekuwa kambi ya mafanio makubwa kwetu” amesema Dkt.Park na kuongeza kuwa

“Tulikuwa na wakati mzuri hapa Tanzania katika kambi ya upasuaji wa mgongo kwa njia ya matundu uliofanyika MOI ambapo kwa kipindi cha siku tatu wagonjwa 12 wamefanyiwa upasuaji huo.”

Kabla ya upasuaji huo kwa njia ya matundu MOI imekuwa ikitoa matibabu kwa kufanya upasuaji wa uti wa mgongo kwa kufunua eneo kubwa hali iliyosababisha maumivu kwa wagonjwa na kulazwa wodini siku nyingi.

About the Author

You may also like these