Dkt. Mpoki afunga mafunzo ya watoa huduma za matibabu kwa wagonjwa wa dharura na mahututi

Na Amani Nsello- MOI

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya amefunga mafunzo ya watoa huduma za matibabu kwa wagonjwa mahututi na wa dharuru huku akiwaasa washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia yote waliyojifunza wakati wa mafunzo hayo.

Dkt. Mpoki alifunga mafunzo hayo jana Ijumaa Februari 7, 2025 katika ukumbi wa mikutano uliopo MOI.

Dkt. Mpoki alisema kuwa watoa huduma hao wanapaswa kuzingatia yale yote waliyofundishwa na kuyafuata ili kuleta ufanisi katika sekta ya afya.

“Mafunzo haya ni muhimu kwa sekta ya afya hususani katika idara ya wagonjwa wa dharura na mahututi, skills (maarifa) mliyopata hapa mnatakiwa mkaitumie kwa vitendo katika kuwahudumia wagonjwa ili sasa muweze kuleta tija na ufanisi zaidi katika sekta ya afya” alisema Dkt. Mpoki

Aidha, Dkt. Mpoki aliipongeza taasisi ya EMSA (Kituo cha Mafunzo cha Tiba na Huduma za Dharura) ambayo iliratibu na kuendesha mafunzo hayo na kufanikiwa kupata wakufunzi kutoka Australia ambao waliweza kuwajengea uwezo washiriki wa mafunzo hayo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa ‘Program’ wa EMSA, Ebonny Ford alimshukuru Dkt. Mpoki kwa kuitikia wito na kutenga muda wake na kwenda kufunga mafunzo hayo na kuwaasa washiriki wa mafunzo hayo namna bora ya kutekekeza majukumu yao kwa wagonjwa wa dharura na mahututi.

Mafunzo hayo yaliendeshwa kwa siku 3 na jana Februari 07, 2025 yalifikia tamati ambapo wataalam 50 wanaotoa huduma za matibabu kwa wagonjwa wa dharura na mahututi walijengewa uwezo wakiwemo wataalam kutoka MOI, JKCI, Hospitali ya Taifa Muhimbili, KCMC, Bugando, Hospitali ya Rufaa Mkoa- Mwananyamala, MUHAS, Zanzibar na Aga Khan.

About the Author

You may also like these