Na Mwandishi Wetu MOI, Ijumaa 22 Septemba 2023
Kufuatia ziara ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu kupokea vifaa tiba kutoka Jumuiya ya St. Roch ya nchini Uingereza, menejimenti ya MOI imeeleza kuendelea kujipanga kupanua huduma zake kwa kujenga kituo cha umahiri cha matibabu ya mgongo (Spine Centre) na utengamao (Rehabilitation centre) katika eneo la MOI lililopo Mbweni jijini Dar es Salaam.
Mkurungenzi Mtendaji wa MOI Prof. Abel Makubi amasema kituo hicho cha umahiri kitatumika kutoa huduma kwa Watanzania na wagonjwa kutoka mataifa mengine utakaogharimu Tsh. 164.4 bilioni.
Amesema taratibu za upembuzi yakinifu zimekamilika na matarajio ni kwamba serikali kupitia Wizara ya Fedha na Wizara ya Afya zitakamilisha mchakato huo mapema ili ujenzi uanze.
Prof. Makubi amesema sambamba na ujenzi huo menejimenti ya MOI inakamilisha utaratibu wa kujenga jengo jipya la wagonjwa wa nje (OPD) ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika eneo la wagonjwa wan je la (OPD) la sasa.
“Mradi huu unatarajia kugharimu sh. 800 milioni hadi 1 bilioni, jengo hilo litakuwa na vyumba zaidi ya 20 vya madaktari vya kuwaona wagonjwa” alisema Prof. Makubi
Amesema hatua hiyo ni katika utekelezaji wa maagizo ya serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha watanzania na raia wa mataifa mengine wanapata huduma bora za kibingwa hapa nchini bila kulazimika kufuata huduma hizo nje ya nchi..