Na Amani Nsello- MOI
Ndugu wa wagonjwa wameeleza kuridhishwa kwao na huduma za matibabu zinazotolewa na Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) na kushauri hospitali za wilaya kuiga mfano wake.
Ombi hilo limetolewa leo Ijumaa Desemba 27, 2024 na baadhi ya ndugu wa wagonjwa walipokuwa wakitoa maoni katika taasisi ya MOI eneo la kusubiria huduma (MOI Clients’ Lounge).
Ndugu wa mgonjwa, Hamida Mnyelele amesema kuwa huduma za matibabu za MOI ni nzuri na za kuridhisha na ameomba pia hospitali za wilaya ziweze kuboresha huduma zake kuanzia huduma kwa wateja hadi masuala ya vipimo.
“Niwapongeze kwa huma zenu nzuri za matibabu, kiukweli huduma za hapa (MOI) na kule tunapotoka kabla ya kufika hapa ni tofauti sana, unaweza kupeleka mgonjwa wako ukifika unaambiwa kifaa cha kipimo kimeharibika, unarudi nyumbani na mgonjwa wako hajahudumiwa”- amesema Bi. Hamida na kusisitiza
“Kule wilayani kuna changamoto sana, hata huduma kwa wateja sio nzuri kulinganisha na hapa MOI, naombeni mfukishe maoni yetu Wizara ya Afya iboreshe huduma kule grass root hali sio nzuri, kule grass root ndo kuna wagonjwa wengi wanaopatiwa huduma za matibabu tofauti na huku ngazi ya Kitaifa”
Kwa upande wake, Meneja wa Fedha wa MOI, Wendelin Ngonyani amesema kuwa wamechukua ushauri wa kuboresha huduma za matibabu katika hospitali za wilaya na wataufikisha Wizara ya Afya.
“Niwaambie tu kuwa ushauri wenu tumeuchukua na tutaufikisha Wizara ya Afya, maana ushauri wenu ni wa muhimu sana katika kuboresha ustawi wa jamii na afya kwa umma… Hivyo niwatoe wasiwasi ushauri utafika kabisa”-amesema Ngonyani
Taasisi ya MOI kupitia Menejimenti yake imentenga siku za Jumatano na Ijumaa kuanzia saa 5 asubuhi hadi saa 6 mchana kwa ajili ya kupokea maoni changamoto, kero na pongezi kutoka kwa wagonjwa na ndugu wa wagonjwa wanaopatiwa huduma za matibabu katika taasisi hiyo.