Na Lissah Besta-MOI
Ndugu wa wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wameombwa kuzingatia usafi na kutunza miundombinu ya taasisi ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa wagonjwa.
Rai hiyo imetolewa leo Agosti, 23, 2024 na Meneja wa wa Utawala wa MOI, Amir Mkapanda wakati wa kusikiliza maoni, kero, ushauri na pongezi kutoka kwa wateja ambapo amesisitiza kuwa ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha huduma zinaendelea kuwa bora.
“Mwenzetu hapa amelalamika matumizi mabaya ya sinki za kuoshea vyombo, lakini si hivyo tu, tumeshuhudia uharibu wa miundombinu pia, wapo waliojaribu kuharibu koki za maji…niwaombe tutambue usafi na kutunza miundombinu ni jukumu la kila mmoja wetu” amesema Mkapanda
Kwa upande wake Marry Chiwale licha ya kuipongeza MOI kwa kutoa huduma bora kwa wateja, pia amewaomba ndugu wa wagonjwa kuzingatia usafi watumiapo miundombinu ya hospitalini hapo.
“Changamoto yangu ni kwa sisi wauguzi, unakuta kwenye sinki la kuoshea vyombo kuna mabaki ya chakula hadi imeziba, kwa kweli hii sio sahihi…usafi ni jukumu letu sote” amesema Chiwale
Kusikiliza maoni, ushauri na changamoto ni zoezi endelevu lenye lengo la kuboresha huduma kwa kupata mrejesho wa ubora wa huduma kutoka kwa wateja.
