Na Stanley Mwalongo-MOI
Ndugu wa wagonjwa wanaopatiwa matibabu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wameipongeza menejimenti na wafanyakazi wa taasisi hiyo kwa kutoa huduma bora kwa wagonjwa.
Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Mei, 3, 2024 wakati wa kutoa maoni, kero, ushauri, changamoto na pongezi ikiwa ni utekelezaji wa adhma ya Taasisi ya kutatua kero za wateja wake kwa wakati ili kuboresha huduma, ndugu hao wamesema wameridhishwa na huduma wanazopewa wagonjwa wao.
“Hata usipokuwapo wodini lakini ukirudi unamkuta mgonjwa wako amehudumiwa katika hali ya upendo kabisa, mazingira mazuri, shuka nzuri kwa kweli moyo unakuwa na amani kuwa mgonjwa wangu yupo sehemu sahihi na salama, hongereni sana kwa kutoa huduma bora” amesema Magreth Chiro
Ndugu mwingine wa mgonjwa Loda Joseph amesema “Madaktari na wauguzi wanafanya kazi nzuri na kwa moyo wa upendo, sina budi niwapongeze kwa huduma nzuri, Mungu awabariki sana”
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Marry Kayora amewashukuru ndugu wa wagonjwa hao kwa pongezi hizo na kusisitiza kuwa Taasisi inaendelea na maboreshao ya huduma ili kukidhi mahitaji ya mgonjwa.
“Kwa sasa hospitali yetu ina madaktari bingwa 75, madaktari bingwa wabobezi 26 na madaktari wa kawaida 49 hii yote ni katika uboresha huduma zetu kwa wagonjwa…hata hivyo taasisi inaendelea kuajiri madaktari na watoa huduma wengine ikiwa ni sehemu ya uboreshaji huduma zetu” amesema Kayora
Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa MOI, Patrick Mvungi amesema taasisi hiyo imejiwekea utaratibu wa kukutana na kupokea maoni, ushauri, changamoto, kero na pongezi kutoka kwa wateja wake kila siku ya Jumatano na Ijumaa kuanzia saa 5:00 asubuhi, na kwamba wateja wasisite kuwasiliana na viongozi pindi wanapopata changamoto yeyote kwa utatuzi wa haraka.
