MOI yapokea vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi bilioni 3 kutoka Uingereza.

Na Mwandishi Wetu – MOI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu ametembelea Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) ambapo kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Ummy Mwalimu amepokea msaada wa vifaa tiba vya upasuaji kutoka Jumuiya ya St. Roch ya nchini Uingereza wenye thamani ya shilingi bilioni 3.

Katika hafla ya kupokea vifaa hivyo na uzinduzi wa kambi ya siku nane ya matibabu iliyofanyika leo Septemba 21, 2023, Ukumbi wa MOI jijini Dar es Salaam Dkt. Jingu ameishukuru Jumuiya ya St. Roch na madaktari hao kwa msaada wa vifaa tiba na kuongeza kuwa utasaidia kuboresha huduma kwa taasisi hiyo.

Alisema vifaa hivyo vitatumika katika upasuaji wa kubadilisha nyonga na magoti, urekebishaji wa misuli ya magoti kwa njia ya matundu, urekebishaji wa ulemavu kwa watoto na upasuaji wa tishu (soft tissue surgery) pamoja na huduma nyingine za kibingwa.

“Msaada mlioutoa ni mkubwa sana, amesema Mkurugenzi Mtendaji (MOI) hapa kuwa una thamani yake ni shilingi bilioni 3, hii si hela ndogo, msaada huu utasaidia kupunguza changamoto ya vifaa tiba vya upasuaji hapa MOI,” alisema Dkt. Jingu

Akizungumzia kambi ya matibabu Katibu Mkuu huyo alisema itasaidia kukuza ujuzi kwa madaktari wazawa na kwamba fursa hiyo italeta matokeo chanya katika utoaji tiba kwa wananchi.

“MOI hii baada ya siku nane, wageni wakiondoka haitakuwa MOI hii, kutakuwa na mabadiliko makubwa sana, hii ni fursa ya kila mmoja kujifunza, fursa hii itatoa matunda chanya na ya kudumu kwa jamii yetu” alisema Jingu.

“MOI ni kituo cha umahiri sio tu kwa Tanzania lakini pia katika ukanda huu, unaenda kuimarisha pia ushirikiano baina ya Tanzania na Uingereza, matarajio yangu kwamba ushirikiano huu baina ya Taasisi yetu ya MOI na Jumuiya ya madaktari bingwa wa mifupa kutoka Uingereza utakuwa endelevu na wenye tija kawa manufaa ya watanzania wote,” alisisitiza Dkt Jingu.

Alisema kwa kutambua kazi bora inayofanywa na MOI ya kutoa huduma za tiba za kidaktari bingwa kwa mifupa na ubongo, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 2 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba mwaka wa fedha 2023/24.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Prof. Abel Makubi ameishukuru Jumuiya ya St. Roch ya nchini Uingereza kwa msaada wa vifaa tiba vya upasuaji na kwamba vifaa na ujio wao utaleta matokeo chanya kwa MOI.

“Kwa niaba ya MOI nawashukuru, karibuni MOI hii ni hopsitali ya Taifa ya tiba ya mifupa, ubongo na ajali, tunatambua jitihada zetu katika kuasisi ushirikiano huu wa kudumu” amesema Prof. Makubi

Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema msaada huo wenye thamani ya shilingi bilioni 3 utaongeza idadi ya wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji kwa siku kutoka wastani wa wagonjwa 24 hadi 42.

“Lengo la hii Kambi ni kutoa huduma za kitabibu za kibingwa kwa wagongwa wetu kwa sasa MOI inakabiliwa na msongamano wa wagonjwa wa nje na ndani na katika kukabiliana na hili tunatajaria kujenga jingo la wagonjwa wa nje,” alisema Makubi.

Kiongozi wa madaktari hao Dkt. Adil Ajuied amesema lengo ni kubadilishana uzoefu na madaktari wa MOI katika tiba za mifupa, viungo, majeraha sungu na ajali.

Alisema wamefarijika kwa mapokezi waliyoyapata na kwamba ni imani yao ushirikiano huo utaendelea katika kujengeana uwezo wa kiujuzi kutokana na kukua kwa technolojia za kitabibu.

About the Author

You may also like these