Na Abdallah Nassoro-MOI
Menejimenti ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imewaomba ndugu wa wagonjwa kuitumia vizuri menejimenti ya Hospitali hiyo pindi wanapowatembelea ndugu zao hospitalini hapo kupata ufafanuzi iwapo watakuwa na malalamiko au ushauri wa kuboresha huduma.
Ombi hilo limetolewa leo Februari 7, 2024 na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Prof. Abeli Makubi wakati wa kusikiliza maoni, kero, ushauri na pongezi ikiwa ni utekelezaji wa utaratibu wa taasisi wa kupata mrejesho wa huduma wanazotoa kutoka kwa wateja wao.
Prof. Makubi amesema ndugu wa mgonjwa au mgonjwa anapaswa kufuata utaratibu wa kuwasilisha maoni, kero au ushauri wowote kwa uongozi ili kupata ufafanuzi badala ya kulalamika kwa watu wa nje ya taasisi.
“Ndugu fuateni utaratibu mnapofika kuona wagonjwa, unapopatwa na changamoto watafuteni viongozi kwa kuwapigia simu au kama hawapokei tumeni meseji kwa Afisa wa Menejiment au kundi wazi la whatsaap la huduma kwa wateja la MOI ili ipatiwe ufumbuzi kwa haraka na si kuwapigia watu nje ya taasisi” kwa sababu menejiment ipo kwa ajili yao na iko karibu nao; amesema Prof. Makubi na kuongeza
“Tupo tayari kupokea mapungufu yetu ili tujirekebishe na tupo tayari kuwahudumia…Ndugu wanatakiwa kufahamu kuwa sio ndugu wote wanapaswa kufahamu taarifa za siri za mgonjwa…mgonjwa anayo haki ya kuchagua watu wa kupewa taarifa za siri za ugonjwa wake na ni hao tu watakaopewa na daktari anapaswa kuheshimu hilo”
Aidha aliwakumbusha ndugu na wagonjwa kuwa walinzi wa mali za taasisi kwa kutoa taarifa pale watakapobaini wizi au uharibifu wa mali za taasisi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu, Orest Mushi amesema menejitimenti imejipanga kuhakikisha inatatua changamoto wanazopata wateja wakati wa kupata huduma na kwamba ni wajibu wao kuwa huru kuwasilisha maoni yao.
Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi Fidelis
Minja amesema wateja wanapwaswa kuwaripoti kwa viongozi wa MOI watoa huduma wanaotumia lugha chafu kwa wateja ili wachukuliwe hatua.
Victor Salum ni mgonjwa anayepata matibabu MOI, licha ya kuipongeza kwa huduma bora alishauri kuboresha mfumo wa upashanaji taarifa pindi daktari anapopata dharura ili kuepusha wagongwa kukaa muda mrefu bila ya kupata huduma.