MOI yahimiza wananchi kujiunga na bima ya afya.

Na Abdulaziz Seif-MOI Alhamisi, Oktoba 5, 2023

Menejimenti ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imewashauri Watanzania kujenga utamaduni wa kujiunga na Mifuko ya Bima ya Afya ili waweze kutibiwa kwa urahisi mara wanapoungua au kupata ajali.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Prof. Abel Makubi akizungumza na wagonjwa na ndugu wa wagonjwa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja leo Alhamisi Oktoba, 5, 2023 amesema uzoefu kutoka taasisi hiyo unaonesha kuwa wagonjwa wengi hajajiunga na mifuko ya bima ya afya hali inayosababisha kuomba msaada wa matibabu pindi wanapoungua.

“Wagonjwa wengi wanaomba watibiwe kwa msamaha, na hii ni kwasababu hawawezi kumudu gharama za matibabu…watu hawa wangekuwa na bima ya afya wangeweza kutibiwa kwa urahisi” amesema Pro. Makubi na kuongeza

“Niwaombe wananchi kujiunga na mifuko ya bima ya afya ili wanapougua basi mifuko hii igharamie matibabu yenu…ni muhimu sana kwasababu unaweza kuugua au kupata ajali wakati ukiwa huna pesa tasilimu ukashindwa kutibiwa kwa wakati”

Baadhi ya wagonjwa hospitalini hapo wameupongeza uongozi wa MOI kwa kuboresha utoaji wa huduma sambamba na kuweka mazingira safi ya utoaji huduma.

“Tunashukuru kwa huduma nzuri, kuna wakati huwezi kuamini kama hospitali za serikali zinaweza kutoa huduma bora kiasi hiki…tofauti na maeneo mengine hali ya usafi hapa ni nzuri sana, nawapongeza kwa hilo” amesema Keza Kaheze

About the Author

You may also like these