MOI yaadhimisha siku ya watoto wenye utindio wa ubongo duniani kwa kufanya uchunguzi bure kwa watoto wenye changamoto hiyo

Na Amani Nsello- KINONDONI

Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeshiriki katika maadhimisho ya siku ya watoto wenye mtindio wa ubongo duniani kwa kwa kufanya uchunguzi bure kwa watoto wenye changamoto hiyo na kutoa elimu ya malezi, makuzi bora na namna ya kuzuia.

Hafla hiyo imefanyika leo Jumapili Oktoba 06, 2024 katika shule ya Kimataifa ya Genesis iliyopo Oysterbay, Kinondoni, Jijini Dar es Salaam ambapo MOI ilishirkiana na wadau wengine.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Daktari bingwa na mbobezi wa upasuaji wa mifupa na ubongo kwa watoto kutoka MOI, Bryson Mcharo amesema kuwa wanawake wajawazito wanatakiwa kuhudhuria kliniki, kuepuka matumizi ya pombe kupindukia na kujikinga na maambukizi kwenye njia ya uzazi ili kuepuka kuzaa watoto wenye mtindio wa ubongo.

“Wanawake wanapohisi ujauzito wanatakiwa kuhudhuria kliniki, pia hata kabla ya ujauzito wanaweza kwenda kwa wataalam na akapewa elimu ya uzazi, kutotumia pombe kupindukia wakati wa ujauzito wajiepushe na ngono zembe maana hupelekea maambukizi kwenye njia ya uzazi mfano gono na kaswende, lakini pia kuepuka matumizi holela ya dawa za binadamu”. Amesema Dkt. Mcharo

Awali akifungua hafla hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saad Mtambule amesema kuwa Manispaa ya Kinondoni ipo kwenye mchakato wa kuanzisha vituo vya elimu jumuishi ili kuwajengea uwezo watoto wenye utindio wa ubongo kuwezesha ujifunzaji ili kujenga maarifa, stadi na mwelekeo chanya kwa watoto hao.

“Wilaya yetu ya Kinondoni ipo kwenye mchakato wa kuanzisha vituo vya elimu jumuishi, itasaidia sana kuwapa elimu kwa watoto hawa wenye mahitaji maalum, msiwafiche watoto wenye changamoto ya utindio wa ubongo, wapelekeni hospitali wakatibiwe”. Amesema Mhe. Mtambule

Maadhimisho hayo ya Siku ya Watoto wenye utindio wa ubongo duniani yalitanguliwa na kambi maalum ya uchunguzi na matibabu ya watoto hao katika taasisi ya MOI.

About the Author

You may also like these