Na Amani Nsello-MOI
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeadhimisha siku ya Fiziotherepia Duniani mwaka 2024 kwa kutoa huduma na elimu kwa wananchi bure, huku wataalam wakishauriwa kuongeza ubunifu katika kutoa huduma bora.
Kilele cha maadhimisho hayo yamefanyika leo Septemba 7, 2024 ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi MOI Dkt. Asha Abdullah ambaye amesisitiza umuhimu wa wataalam wa Fiziotherapia wa Taasisi ya MOI kuendelea kutoa huduma bora zaidi na kuongeza ubunifu , ili kutekeleza maagizo na maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hasaan ya kuhakikisha huduma za afya nchini zinakuwa bora.
“Leo tunaadhimisha siku ya Fiziotherapia duniani sisi kama wataalamu wa mazoezi tunatakiwa kutoa huduma bora zaidi na ya ziada kwani hayo ni maagizo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunatakiwa kuhakikisha tunatoa huduma bora kwa Watanzania na kuongeza ubunifu katika huduma zetu za matibabu za Fiziotherapia” amesema Dkt. Asha
Kwa upande wake Afisa Fiziotherapia wa MOI, Emmanuel Ngwiza ameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuendelea kutoa vifaa tiba vya kisasa , kwani vinawarahishia utoaji wa huduma za kimatibabu kwa wagonjwa wanaohitaji mazoezi tiba na viungo.
“Tunaishukuru sana serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa mchango mkubwa katika sekta ya afya hususani katika Taasisi ya MOI kwa vifaa tiba na kutusomesha sisi wataalam kwani vinatutahisishia katika utendaji kazi wetu” amesema Emmanuel
Maadhimisho hayo ya mwaka 2024 yenye kauli mbinu “ Umuhimu wa Fiziotherapia katika kuzuia na kutibu maumivu ya mgongo” yalitanguliwa na ushauri kutoka kwa wataalamu wa Fiziotherapia kutoka MOI sambamba na kliniki ya Fiziotherapia kwa wananchi bure.