MOI kuboresha mfumo wa utoaji wa taarifa kwa ndugu wa wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji.

Na Abdallah Nassoro

Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imejipanga kuboresha utoaji wa taarifa za mwenendo wa upasuaji wa wagonjwa kwa ndugu wa wagonjwa wao mara wanaopingizwa katika chumba cha upasuaji .

Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Machi, 13, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Mhe: Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya wakati akitoa taarifa yake kwa kikao cha kwanza cha baraza la sita la wafanyakazi kinachoendelea katika hoteli ya Edema mjini Morogoro.

Amesema kitengo cha teknolojia ya habari (ICT) kipo katika hatua za mwisho za kuandaa mfumo utakaomwezesha ndugu wa mgonjwa anayefanyiwa upasuaji kupata taarifa juu ya hatua zote ambazo mgonjwa wake atakuwa amefanyiwa akiwa katika chumba cha upasuaji.

“Mfumo huu utamjulisha ndugu wa mgonjwa hatua zote ambazo mgonjwa anapitia kwa wakati husika” amesema Dkt. Mpoki na kuongeza kuwa

“Hatutaki ndugu wa mgonjwa aanze kupiga simu kwa madaktari chumba cha upasuaji kuuliza maendeleo ya mgonjwa wake, hatutaki ndugu wakae karibu na ‘theater’ kusubiri maendeleo ya mgonjwa…ndugu anaweza kukaa nyumbani lakini akawa na taarifa zote za maendeleo ya upasuaji”

Aidha Dkt. Mpoki alitumia fursa hiyo kuwapongeza watumishi wote wa MOI kwa kazi nzuri ambazo zimechangia kuifanya MOI kuwa taasisi bora ya matibabu barani Afrika, na kwamba kuna kila sababu ya kupanua wigo wa kurithisha taaluma hiyo kwa vizazi vingine.

“Nawapongeza watumishi wote wa MOI kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kutoa huduma bora kwa wagonjwa wetu , endeleeni kufanya kazi kwa bidii na kwa uzalendo”

“Tunatakiwa kupanua ushirikiano wetu na vyuo vikuu ili MOI iwe sehemu ya kutoa taaluma kwa wanafunzi wa udaktari na uuguzi” Amesema Dkt. Mpoki

Kwa upande wake mwenyekiti wa TUGHE tawi la MOI, Privatus Masula licha ya kuupongeza uongozi wa MOI kwa kuendelea kuboresha maslahi ya watumishi, pia ameomba menejimenti kuanza kutekeleza waraka mpya wa posho za watumishi ili kuongeza ari ya watumishi kufanya kazi.

“Mhe: Mwenyekiti tangu waraka mpya wa posho za watumishi utolewe miaka miwili iliyopita bado taasisi haijaanza kuutekeleza, ni wakati sasa kwa watumishi hao kuanza kulipwa posho zao kwa kuzingatia waraka huo mpya” amesema Masula

Kikao cha kwanza cha baraza la sita la wafanyakazi wa taasisi ya MOI kinaendelea kwa siku mbili ambapo wajumbe watajadili na kufanya maamuzi ya mambo mbalimbali ya ustawi wa taasisi hiyo.

About the Author

You may also like these