Mhe. Mhagama akoshwa na wataalam wa MOI wanavyohudumia wagonjwa kutoka mataifa ya nje

Na Erick Dilli-Dodoma

Waziri wa Afya Mhe. Jenister Mhagama[Mb] amesema amefurahishwa na namna ambavyo watumishi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wanavyofanya kazi ya kuwahudumia wagonjwa wanaotoka nje ya nchi.

Katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Afya Kitaifa yanayofanyika Mkoani Dodoma Aprili 08, 2025 Mhe. Mhagama ametembelea banda la MOI na kuelezea furaha yake kwa namna taasisi hiyo wanavyohudumia wagonjwa wanaotoka nje ya nchi.

‘’Napendezwa na namna mnavyotoa huduma za kibingwa na kibobezi kwa wagonjwa kutoka mataifa ya nje, niwahisi muendelee kutoa huduma hizo ili mkuze tiba utalii’’ amesema Mhe. Mhagama

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya MOI Balozi Mhe, Dkt. Mpoki Ulisubisya amemuelezea Waziri wa Afya kuwa hadi kufikia Januari mwaka huu jumla ya wagonjwa 6,106 kutoka nje ya nchi waliohudumiwa katika taasisi hiyo.

“Hadi kufikia Januari 2025 tumeweza kuona wagonjwa 6,106 kutoka nchi za nje wenye shida za Mifupa, Ubongo, Mgongo na Mishipa ya fahamu na wengi wanatoka nchi za Comoro, Zambia, Malawi na wengine kutoka ndani na nje ya Afrika” amesema Dkt. Mpoki na kuongezea

“Wagonjwa hawa huwa wanapata huduma yenye kiwango cha Kimataifa katika kliniki yetu ya ‘Premier and International Patient Services’ ambapo kuna mandhari nzuri na kuhudumiwa kwa muda mfupi ili waendelee na shughuli zao’’

Taasisi ya MOI ilianza rasmi kutoa huduma za wagonjwa maalum na wa kimataifa mnamo Oktoba 2023 kwa dhumuni la kukuza na kuendeleza tiba utalii ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

About the Author

You may also like these