Na Abdallah Nassoro- ZANZIBAR
Wananchi wa visiwani Zanzibar wameipongeza na kuishikuru Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kwa kutoa matibabu ya kibingwa ya Mifupa, Ubongo, mgongo, mishipa ya fahamu, magonjwa ya ndani na fizotherapia bure katika kambi maalum ya matibabu iliyoratibiwa na Idara ya Habari Maelezo.
Wananchi hao wamesema uwepo wa Kambi hiyo imewarahisishia kupata matibabu ya kibingwa karibu yao na kuwapunguzia gharama za kusafiri hadi jijini Dar es Salaam kufuata huduma hizo.
“Isingekuwa rahisi kwetu sisi kufuata huduma hizi Dar es Salaam, lakini kwa Kambi hii tunaishukuru na kuipongeza MOI kwa jitihada hizi za kutusogezea huduma za kibingwa karibu nasi” amesema Bi, Habiba Abdallah mkazi wa Unguja visiwani Zanzibar
“Tunaishukuru serikali yetu na waratibu wa jambo hili kwa kuwezesha uwepo wa Kambi hii, tunapata na dawa pia jambo ambalo ni faraja kwetu, ila tunaomba siku zingeongezwa kwasababu wagonjwa tupo wengi na siku za huduma ni chache” ameongeza Bi. Abdallah
Mkazi mwingine Ismail Juma amesema uwepo wa kambi hiyo maalum ya matibabu imewezesha wananchi wenye kipato cha chini kupata matibabu bure.
“Sisi wenye kipato Cha chini tumeguswa mno na hii Kambi kwasababu tumeweza kupata matibabu tena ya kibingwa, hakika ni faraja kwetu, tunawapongeza kwa huduma bora” Bw. Juma
Taasisi ya MOI imeendesha Kambi maalum ya matibabu kwa wananchi visiwani Zaznibar kwa siku 4 mfululizo ikiwa ni sehemu ya kikao kazi Cha 20 Cha Maafisa Habari wa Serikali kilichomalizika Aprili, 6, 2025.