Na Abdallah Nassoro-MOI
Menejimenti ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imesema kuwa bado haijaridhishwa na kiwango cha ubora wa huduma kwa wateja licha ya wagonjwa wanaopatiwa matibabu hospitalini hapo kufurahishwa na huduma hizo.
Hayo yamesemwa siku ya Jumatano Septemba 04, 2024 na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya MOI Dkt. Lemeri Mchome wakati akizungumza na wagonjwa pamoja na ndugu wa wagonjwa wakati wa zoezi la kusikiliza kero, maoni, ushauri na changamoto katika banda la kupumzika wateja la MOI mpya.
Dkt. Lemeri amesema kuwa anashukuru kwa sasa hakuna mgonjwa au ndugu wa mgonjwa ambaye amelalamikia huduma za kimatibabu zinazotolewa MOI, lakini bado kama Menejimenti haijaridhishwa na huduma zinazotolewa licha ya kuwa wagonjwa wanafurahishwa na huduma hizo.
“Tunashukuru hakuna mgonjwa wala ndugu wa mgonjwa ambaye ametoa malalamiko ya huduma za matibabu zinazolewa hapa MOI, pengine tulimtibu vibaya au kusubirishwa muda mrefu kusubiri huduma. Wengi mmetusifia kuwa tunatoa huduma bora, lakini sisi kama taasisi bado hatujaridhika tutaendelea kuongeza ubunifu ili tuendelee kutoa huduma bora zaidi za kimatibabu”. amesema Dkt. Lemeri
Mmoja wa ndugu wa mgonjwa, Ali Juma ameipongeza MOI kwa huduma bora za matibabu “Nipende kutoa shukurani kwa huduma zenu hapa MOI, ni nzuri wala sijapata changamoto yoyote ya matibabu tangia nimefika hapa”. amesema Juma
Menejimenti ya Taasisi ya MOI imetenga siku za Jumatano na Ijumaa kwa ajili ya kusikiliza kero, maoni, mapendekezo, ushauri na pongezi kutoka kwa wagonjwa na ndugu wa wagonjwa. Jukwaa hili limekuwa msaada mkubwa kwa menejimenti ya taasisi kupata mrejesho wa huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo.
