Mamia ya wananchi zanzibar wajitokeza kupata huduma za kibingwa MOI

Na Abdallah Nassoro- ZANZIBAR

Mamia ya wananchi wa visiwani Zanzibar wamejitokeza kwa wingi kuapata huduma za kibingwa za mifupa, ubongo, mgongo, mishipa ya fahamu, magonjwa ya ndani na fiziotherapia zinazotolewa na Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Mihimbili (MOI) katika kambi maalum ya matibabu ya siku nne yaliyoambatana na kikao kazi cha 20 cha Maofisa Habari Serikalini kinachoendelea Viwanja vya Amaan visiwani hapa.

Ikiwa ni siku ya pili ya kutolewa kwa huduma hizo bure kwa wananchi na washiriki wa kikao hicho, wananchi wengi wameonesha kuguswa na huduma za kibingwa zinazotolewa na MOI na kujitokeza kwa wingi kupata huduma.

Daktari bingwa wa mifupa wa MOI, Dkt. Tumaini Minja amesema kwa siku ya kwanza jumla ya wagonjwa 108 walipata huduma za matibabu ya kibingwa kutoka kwa wataalam na kwamba idadi hiyo inatarajia kuongezeka mara dufu kwa siku ya pili.

“Jana Aprili 3, 2025 siku ya kwanza ya kambi ya matibabu hapa Zanzibar tumefanikiwa kuwaona wagonjwa 108 ambapo wamepata huduma za kibingwa za mifupa, ubongo, mgongo, magonjwa ya ndani na fiziotherapia” amesema Dkt. Minja na kuongeza kuwa

“Mwamko wa wananchi kujitokeza kupata huduma zetu za kibingwa ni mkubwa na tunatarajia kadri siku zinavyokwenda ndivyo idadi ya wagonjwa inavongezeka…kwetu ni fahari kuwasogezea huduma hizi za kibingwa karibu na wananchi na bila malipo”

“Wengi tuliowaona wana matatizo ya mgongo, nyonga na magoti…tumewapa ushauri na dawa, na kwa wale ambao changamoto zao ni kubwa tumewapatia rufaa ya moja kwa moja kwenda MOI” amesema Dkt. Minja

About the Author

You may also like these