MAMIA WAJITOKEZA KUCHANGIA DAMU MOI WAPEWA ELIMU YA UMUHIMU WA BIMA YA AFYA KWA WOTE

Mamia wajitokeza kuchangia damu MOI wapewa elimu ya umuhimu wa bima ya afya kwa wote

Na Mwandishi wetu- MOI

Mamia ya Wanafunzi kutoka vyuo vikuu na kati vya jijini Dar es Salaam wamejitokeza kwa wingi kuchangia damu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa MOI pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili kwaajili ya kusaidia wagonjwa wenye uhitaji wa damu ambapo zaidi ya chupa 300 za damu zimepatikana kupitia zoezi hilo.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respicious Boniface amesema MOI inatumia chupa 25 mpaka 30 ambapo kwa wiki zinahitajika chupa 150 za damu.

“MOI inatoa matibabu ya kibingwa na kibobezi ya upasuaji wa Mifupa, Ubongo, Mgongo na Mishipa ya fahamu hivyo kuna uhitaji wa damu ni mkubwa hivyo  damu iliyopatikana inakwenda kuwasaidia wagonjwa wanaohitaji wa upasuaji na waliolazwa wodini ” alisema Dkt. Boniface.

Aidha Dkt.Boniface ameushukuru uongozi wa Vyuo Vikuu Vya Tanzania (TAHLISO) na Mdau wa Afya Azim Dewji kwa kufanikisha zoezi hili la uchangiaji damu wa hiari.

Kwaupande wake Mfanyabiashara Azim Dewji amesema damu haitengenezwi kiwandani hivyo anawasihi  Watanzania waendelee kujitokeza kwa wingi kuchangia damu ili kuwasaidia watu wenye uhitaji.

“ Nawashukuru wote mliochangia damu kwani haina kiwanda duniani, haina kabila na wala itikadi kwahiyo unapochangia damu zinaenda kuokoa maisha ya watu wenye uhitaji hospitalini” alisema Bw.Dewji.

Mwanafunzi wa Chuo cha Ustawi wa Jamii Bi. Fatma Joseph amesema amekuja kuchangia damu MOI kwasababu Taasisi ya MOI inapokea wagonjwa wengi  wenye uhitaji wa damu na pia amewahamisha wanachuo wenzake wachangie damu ili kuokoa maisha ya wagonjwa.

Elimu ya bima ya afya kwa wote ilitolewa na timu ya wataalum kutoka Taasisi zilizopo chini ya wizara ya afya na kuwataka wanafunzi hao wakawe mabalozi kwa wenzao.

About the Author

You may also like these