Kitengo cha dharura MOI wahimizwa kuimarisha ushirikiano kuokoa maisha ya majeruhi.

Na Mwandishi Wetu, MOI-Tarehe 17 Agosti, 2023

Wataalam na wahudumu wa kitengo cha dharula na uthibiti majeruhi katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) wamehimizwa kufanya kazi kwa ushirikiano ili kupunguza vifo vinavyozuilika, ulemavu unaotokana na majeruhi na madhara ya upasuaji makubwa.

Wito huo umetolewa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Prof. Abel Makubi wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya maboresho ya huduma ya dharura na udhibiti wa majeruhi wa ajali yanayoendelea MOI.

Amesema iwapo watumishi wa kitengo hicho watafanya kazi kwa ushirikiano wataweza kuboresha huduma zaidi na kunusuru vifo vitokanavyo na ajali.

“Tangu mwaka 2006 tumekuwa na jitihada za pamoja kufikia lengo la kupunguza vifo vinavyozulika na ulemavu unaotokana na majeruhi na maradhi yatokanayo na upasuaji mkubwa, malengo haya yatatimia kwa watumishi kufanya kazi kwa pamoja” alisema Prof. Makubi

Alibainisha kuwa “Ushirikiano uliopo baina ya MOI na Kituo cha Kimataifa cha Upasuaji cha Chuo Kikuu cha McGill (CGS) cha nchini Canada si tu kimegusa maisha ya watu bali pia umeonesha uwajibikaji katika kubadilishana mitazamo na ujuzi”.

Mratibu wa mafunzo hayo Dkt. Victoria Munthali amesema lengo ni kuwajengea uwezo watumishi wa kitengo cha dharura ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi na kupunguza vifo vinavyozuilika vinavyotokana na ajali.

“Mafunzo haya tumeshirikiana na Kituo cha Kimataifa cha huduma za upasuaji kilichopo chuo kikuu cha McGill cha nchini Canada, tunataka mgonjwa apate huduma bora na kwa wakati”

About the Author

You may also like these