JOPO LA WATAALAM WA MOI

Jopo la wataalam kutoka MOI lafanya tathmini Hospitali ya rufaa kanda ya kusini Mtwara

Wizara ya Afya kupitia Taasisi ya MOI imetuma jopo la wataalamu kufanya tathmini katika hospitali ya rufaa ya kanda ya kusini Mtwara ili kuangalia maboresho muhimu kabla ya huduma za kibingwa za MOI pamoja na huduma nyingine kuanza kutolewa hospitalini hapo hivi karibuni.

Jopo la wataalam limehusisha Daktari Bingwa wa upasuaji wa ubongo, Mgongo na mishipa ya fahamu, daktari bingwa wa mifupa wa watoto, Daktari bingwa wa kutoa dawa za usingizi na ganzi, Muuguzi mbobezi wa chumba cha upasuaji pamoja na Mhandisi.

Wataalam hao wamepokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Ahmed Abass ,Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Dunstan Kyobya pamoja na Katibu tawala wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Abdallah Malela ambao katika vipindi tofauti wamepongeza jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali kupitia Taasisi ya MOI za kusogeza huduma za kibingwa kwa wakazi wa mikoa ya kusini na mataifa jirani.

Pamoja na mambo mengine, jopo hilo limepita na kukagua maeneo mbalimbali ya hospitali mpya na ya kisasa ya rufaa kanda ya kusini ili kutoa ushauri wa kitaalam ili huduma za kibingwa na kibobezi za mifupa, mgongo na mishipa ya fahamu pamoja huduma nyingine zianze kutolewa hospitalini hapo.

Hii ni muendelezo wa ziara ya Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface aliyoifanya katika hospitali ya rufaa ya kanda kusini wiki chache zilizopita ili kuangalia namna ya kusogeza huduma za kibingwa kwa wakazi wa Mikoa ya kusini na Mataifa jirani. 

Taasisi ya MOI imekua ikitekeleza kwa vitendo agizo la Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha huduma za kibingwa zinasogwa karibu na Wananchi.

About the Author

You may also like these