12 WAFANYIWA UPASUAJI KWA MBINU YA KISASA

12 wafanyiwa upasuaji wa Ubongo, Mgongo kwa mbinu za kisasa

Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa kushirikiana na Hospitali ya Ramaiah ya Bangalore, India zimeendesha kambi maalum ya uchunguzi na upasuaji wa Ubongo na mgongo kwa mbinu za kisasa ambapo zaidi ya wagonjwa 12 watahudumiwa.

Kambi hii ni matokeo ya  ushirikiano baina ya MOI na hospitali ya Ramaiah ya India ambao umejikita katika tiba, utafiti pamoja mafunzo ya muda mrefu na mfupi.

Mkurugenzi Mtendaji  wa MOI Dkt. Respicious Boniface amesema lengo la kambi hii ya upasuaji ni kuwajengea uwezo Madaktari bingwa wa MOI kwa kuwapa mbinu za kisasa za uchunguzi na tiba ya ubongo kwa kutumia maabara ya kisasa iliyopo MOI pamoja na upasuaji wa ubongo na mgongo.

“Leo ni siku ya pili ya kambi yetu maalum ya uchunguzi na uapasuaji wa ubongo na mgongo kwa kushirikiana na wenzetu kutoka Ramaiah India, jana tuliwafanyia wagonjwa 5 uchunguzi wa ubongo bila kufungua fuvu na wengine 2 watafanyiwa kesho, wagonjwa 3 watafanyiwa upasuaji wa kuondoa vivimbe vya mishipa ya damu kwenye ubongo na wengine 2 watafanyiwa upasuaji wa mgongo kwa kufungua eneo dogo” Alisema Dkt Boniface.

Dkt. Boniface ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mh Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha vifaa tiba vya kisasa vinapatikana hapa MOI na hivyo wagonjwa kutolazimika kufuata huduma hizi nje ya nchi.

Daktari bingwa wa upasuaji wa ubongo kutoka Hospitali ya Ramaiah nchini India  Dkt Sunil Furtado amesema hii ni mara tatu wanakuja kutoa ujuzi  hapa nchini na ameona mabadiliko makubwa kwa wataalamu wa MOI.

Kwaupande wake Daktari bingwa wa upasuaji wa ubongo,mgongo na mishipa ya fahamu MOI, Dkt Lemery Mchome amesema kambi hii imekua na mafanikio makubwa kwa wataalamu wa MOI pamoja na wagonjwa ambao wanapata huduma hapa nchini bila kulazimika kufuata huduma hizo nje ya nchi.

Huu ni mkakati wa Taasisi ya MOI wa kuhakikisha inawajengea uwezo wataalamu wake kwa kuwapa mbinu za kisasa za upasuaji ili waendelee kutoa huduma za kiwango cha juu kwa wananchi.

About the Author

You may also like these