KAMBI NKINGA HOSPITAL

Jopo la Madaktari bingwa wa MOI lapiga kambi katika hospitali ya Nkinga, Tabora

Na Mwandishi wetu- Tabora

Jopo la Madaktari bingwa wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) wamepiga kambi katika hospitali ya rufaa ya Nkinga iliyopo mkoani Tabora, ambapo katika siku kwanza zaidi ya wagonjwa 150 wamehudumiwa katika kambi hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya rufaa Nkinga Bw. Victor Ntundwe amesema kambi hiyo inafanyika kwa siku tano ambapo matibabu ya kibingwa na bobezi yatatolewa kwa wananchi wa kanda ya Magharibi.

“Ushirikiano kati ya MOI na NKinga unalenga kuisaidia serikali kufikia lengo lake la kuwapatia wananchi huduma bora na kwa bei nafuu, pia kuwaondolea adha ya kufuata huduma hizi MOI ambapo wangetumia gharama zaidi kama wangezifuata Dar es Salaam” amesema Ntundwe.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa Nkinga Dkt. Tito Chaula amesema wananchi wa Tabora na mikoa ya jirani wamejitokeza kwa wingi kupata huduma za kibingwa bobezi katika kambi hiyo.

“Siku ya leo tumewahudumia Zaidi ya wagonjwa 150 ambao wengi wao walikuwa wanasumbuliwa na mifupa, magoti, mgongo na watoto wenye vichwa vikubwa, mgongo wazi ambapo kuna baadhi yao tutawafanyia upasuaji kesho” amesema Dkt. Dkt. Chaula

Pia, Daktari bingwa wa Ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu wa MOI, Dkt. John Mtei amesema wanatekeleza agizo la serikali ya awamu ya sita ya kusogeza huduma za kibingwa na bobezi kwa wananchi.

“Tunatoa matibabu na elimu juu ya magonjwa yanayoshambulia mifupa, ubongo , mgongo na mishipa ya fahamu kwa wakazi wa Tabora, Singida, Shinyanga na Kigoma nah ii ni kuhakikisha unatekeleza agizo la Serikali kwa kusogeza huduma zetu kwa wananchi” amesema Dkt. Mtei

Mkazi wa Tabora Bw. Salum Hussein Manua ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusogeza huduma za kibingwa na kibobezi kwani huduma hizo walikuwa wanazifuata Dar es Salaam kwa gharama kubwa .

About the Author

You may also like these