Na Amani Nsello- MOI
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya ametoa rai kwa watumishi wa taasisi hiyo kuendelea kufanya kazi kwa bidii, welei na maarifa wakiweka mbele maslahi ya wananchi wanaopata huduma katika taasisi hiyo.
Dkt. Mpoki alitoa rai hiyo jana Jumatano Januari 29, 2025 katika kikao kazi na watumishi wa Idara ya Huduma za Uuguzi MOI ambapo aliwaasa watumishi hao kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi, maarifa na upendo mkubwa ili kuboresha huduma kwa wateja.
“Endeleeni kuchapa kazi kwa kutoa huduma bora za matibabu kwa wagonjwa wanaofika MOI, ili wakawe mashuhuda kuhusu huduma zetu, pia niombe muendelee kuwa na moyo na ushirikiano ambao mmekuwa nao kwa kufanya kazi kwa bidii bila kuangalia maslahi yenu binafsi bali mkiangalia maslahi ya wananchi”-alisema Dkt. Mpoki
Pia, Dkt. Mpoki aliwaeleza watumishi hao kwamba changamoto zao zote zitafanyiwa kazi kadri rasilimali fedha itakavyopatikana.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wa MOI, Stella Kihombo alimshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa MOI kwa kutenga muda wake na kuandaa kikao kazi hicho na kusikiliza ushauri na maoni ya watumishi hao na kutolea majibu.
“Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa uhai, pili tunamshukuru sana Mkurugenzi wetu, kiongozi wetu kwa kutenga muda wake na kuandaa kikao hiki cha kukutana na sisi (watumishi) na kusikiliza maoni na ushauri wetu kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma hospitalini kwetu” alisema Bi. Stella.