Wagonjwa 600 wafaidika na huduma za kibingwa za MOI nchini comoro

Na Mwandishi Wetu- COMORO (Anjouan)

Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imefanikiwa kutoa matibabu ya kibingwa kwa wagonjwa 600 ndani ya siku tano za kutoa matibabu katika kisiwa cha Anjouan nchini Comoro.

Hayo yalibainishwa Oktoba, 10, 2025 na Kaimu Mwenyekiti wa Utalii Tiba wa MOI Dkt. Joseph Sabas ikiwa ni siku ya tano ya utoaji huduma katika kambi hiyo.

“Tupo madaktari bingwa watatu kutoka MOI, wawili wa mifupa na mmoja wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu, kila mmoja wetu anawaona wagonjwa wastani wa 40 kwa siku, hata hivyo idadi inaongezeka kutokana na uhitaji mkubwa wa huduma zetu” alisema Dkt. Sabas

Aliongeza kuwa “Wagonjwa wa matatizo ya mifupa ni wengi zaidi ukilinganisha na wa ubongo, changamoto za ajali kutokana na uwapo wa miinuko mikubwa na uzee zimekuwa sababu kubwa…tumejipanga kuhakikisha kuwa wagonjwa wote walioandikishwa wanapata matibabu”

Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Saidi Yakubu alisema maendeleo ya kambi hiyo ni mazuri na kwamba zaidi ya wagonjwa 3000 wameandikishwa kwa ajili ya kupata matibabu.

Katika kambi hiyo maalum ya matibabu, inayotarajia kufikia tamati leo Oktoba 11, 2025 MOI imeambatana na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa (MNH), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ya Kansa ya Ocean Road (ORCI) na Hospitali ya Benjamin Mkapa ya Makao Makuu ya nchi Dodoma

About the Author

You may also like these