Na Amani Nsello- MOI
Kampuni ya Bima ya Afya ya Strategies ya Tanzania na Discovery ya Afrika Kusini zimeridhishwa na huduma za kibingwa na za kibobezi zinazotolewa na Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) na kuahidi kuendelea kushirikiana na MOI kwa kuleta wagonjwa wao kupatiwa matibabu.
Hayo yalisemwa jana Alhamis Februari 13, 2025 na Mkuu wa Kitengo cha Biashara wa Kampuni ya Bima ya Afya ya Discovery kutoka Afrika Kusini, Jessica Chivinge walipofanya ziara katika taasisi ya MOI akiambata na viongozi wengine wa kampuni hiyo.
Bi. Jessica alisema kwamba wameridhishwa na huduma za kibingwa na kibobezi zinazotelewa na wataalam wa MOI na kuahidi kuwa wataendelea kutoa ushirikiano na MOI na Strategies kwa kuwaleta wagonjwa wao kutibiwa.
“Kiukweli tumefurahia kuja hapa hospitalini (MOI), tumeona madaktari na wauguzi wanatoa huduma kwa kujituma… Hakika hizi huduma ni za kibingwa na kibobezi… Tumezungushwa maeneo mbalimbali kama kule kwenye vyumba vya Mionzi (X- Ray, CT Scan na MRI) mna vifaa vya kisasa ambavyo vinaubora wa hali ya juu”- alisema Bi Jessica na kuongezea
“Tutaleta wagonjwa wetu hapa (MOI) badala ya kuwapeleka India sasa tutawaleta watibiwe hapahapa MOI, kwa maana tumeridhishwa na huduma zenu”
Naye, Mwakilishi wa Kampuni ya bima ya Afya ya Strategies kwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili- Upanga, MOI na JKCI alisema kuwa wameanza ushirikiano na Kampuni ya Discovery mwaka huu (2025) na katika hatua za awali kampuni hiyo imetuma wawakilishi Tanzania kwa lengo la kuona na kujiridhisha huduma zinazotolewa na taasisi hizo ili sasa mchakato rasmi uanze.
Kwa upande wake, Meneja Udhibiti Ubora wa MOI, Dkt. Paul Kazungu alisema kuwa wao kama MOI wapo tayari kushirikiana na kampuni hiyo kwa kuwapokea wagonjwa wao kutoka Afrika ya Kusini na kuwapatia huduma za matibabu ya kibingwa na kibobezi katika taasisi ya MOI ili kufanikisha dhamira ya serikali ya utalii tiba.