Erick Dilli- MOI
Kanisa la Azania Front kupitia kwaya ya Agape imetoa msaada wa vitu mbalimbali pamoja na kuchangia gharama za matibabu kwa Watoto wenye kichwa kikubwa wanaopata matibabu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI)
Msaada huo umetolewa leo Jumatano tarehe 12, Februari 2025, ukitanguliwa na Maombi pamoja na Nyimbo za kumsifu Mungu.
Katibu wa kwaya hiyo Bw. Michael Nkya amesema huwa ni utaratibu wao kila mwaka kurudisha kwa jamii kwa kile walichobarikiwa.
“Tunamshukuru Mungu kwa kutupa nafasi nyingine ya kuweza kuwepo tena hapa (MOI) na leo tumekuja kutoa msaada kwa watoto wenye kichwa kikubwa na mgongo wazi, tumeleta mafuta, pipi, nepi za watoto na wakubwa, maji, biskuti pamoja na kuchangia gharama za matibabu kwa watoto hawa”
Kwa upande wa Daktari bingwa wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya fahamu Dkt. Hamis Shaban amekishukuru kikundi hiko kwa upendo wao wakuweza kuwasaidia watoto hawa na kutoa rai kwa wadau wengine kuendelea kuchangia matibabu
“Tunashukuru bado mpo na sisi kwa kuendelea kuchangia matibabu ya watoto hawa pamoja na kuja vitu mbalimbali ambavyo vitawasaidia watoto hawa wakati bado wodini” ameongezea
“Nitoe rai kwa wadau wengine kuendelea kusaidia gharama za matibabu kwa watoto hawa kwani wanauhitaji mkubwa wakati wakiendelea kupatiwa matibabu” amesema Dkt.Shaban