Na Amani Nsello-MOI
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeendesha msimu wa nne wa mbio fupi za MOI maarufu kama MOI Marathon kwa lengo la kusaidia matibabu ya watoto 100 wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi na kuzindua kampeni ya kuwafikia watoto wote wanaozaliwa na kichwa kikubwa na mgongo wazi nchini.
Mbio fupi hizo zimefanyika leo Jumapili Septemba 01, 2024 katika uwanja wa MUHAS Muhimbili ambapo takribani washiriki 1500 kutoka nchini Tanzania na Mataifa mbalimbali wameshiriki.
Akimuwakilisha Waziri wa afya, Mkurugenzi wa Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Ahmad Makwani amesema kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anajali afya za Watanzania kwani ametoa fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha na kuendeleza sekta ya afya.
“Ndugu washiriki napenda kuwaarifu kwamba Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ametoa Tsh bilioni 1.5 katika hospitali za Rufaa za Kanda pamoja na MNH, JKCI na MOI ili kuhakikisha kwamba wale wenye mahitaji maalum kama hawa watoto wenye mgongo wazi na vichwa vikubwa wanapata huduma bora na kwa wakati bila pingamizi la fedha”. Ameongezea Dkt. Ahmad
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya tiba ya mifupa na ubongo Muhimbili (MOI) Dkt. Lemeri Mchome amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika muendelezo wa mchango wake mkubwa katika Sekta ya Afya.
“Nimshukuru Rais wetu mpendwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya ya kuendeleza huduma katika sekta ya afya, ikiwa ni sehemu ya huduma katika jamii, tunashukuru kwa mageuzi makubwa katika sekta hii ya afya” Amesema Dkt. Lemeri
Ikumbukwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa mchango wa kusaidia matibabu ya watoto mia wa vichwa vikubwa na mgongo wazi, kwa idadi hiyo itafanya kuwa jumla ya watoto mia mbili kufikiwa na huduma ya matibabu ya vichwa vikubwa na mgongo wazi.
Mh. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan pia alielekeza taasisi ya MOI kuendelea kuzijengea uwezo hospitali za Kanda, Mikoa na Wilaya ili huduma kwa watoto hawa zipatikane mapema na kwa urahisi ili kuwapa nafasi ya kukua kama watoto wengine.
